Lionel Andrés Messi, Lionel Andrés Messi, Lionel Andrés Messi……its Messiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii” Ahsante mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuona talanta hii ya ajabu na ya kipekee ulimwenguni iliyotufanya tuuone mpira ni kitu chepesi kwa macho na kuyafanya yote yasiyowezekana ndani ya uwanja yawe ya kuwezekana ndani ya dakika moja tu.

Kiumbe kilichomfanya Mzee Fergie ambaye alisifika kwa ukauzu, uimara na ukali kwa wachezaji wake pindi walipoonekana kulega lega mchezoni, atetemeke ipasavyo pale Webley Stadium mwaka 2011 kwenye Fainali ya UEFA Champions league mithili ya mwanafunzi aliyeona bakora mikononi mwa Mwalimu mkali. Ni Leo Messi huyu huyu aliyemfanya Mzee Arsene Wenger, adondoke kwa kiti zaidi ya mara mbili kwenye benchi la ufundi la The Gunners kutokana na ukatili uliokuwa ukifanywa na miguu yake wakati akiwaadhibu walinzi wa Arsenal kwa chenga za maudhi.

Kiukweli hiki ni kiumbe kisichoelezeka kwa usahihi hata ukitazame mara ngapi kikiwa kinafanya mambo yake uwanjani, ngoja nimnukuu nguli wa soka wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Brazil Ronaldinho Gaucho wakati akikabidhiwa tuzo ya mchezaji bora wa dunia (Ballon d’Or) mwaka 2005 ikitajwa kuwa ndiyo nyota wa wakati huo ili kurahisisha utata huu.

Tuzo hii inasema mimi ni bora duniani lakini kiukweli mimi si bora ndani ya Barcelona, kuna mtu aliye bora” – alisema Ronaldinho na kuishia juu kwa juu bila kumtaja huyo aliye bora jambo lililoacha maswali vichwani mwa watu wengi lakini nadhani leo hii watu wana majibu ya nani alimaanishwa na Ronaldinho mwaka 2005.

Lionel Messi huyu aliyepelekwa Barcelona kwa lengo Mama la kutibiwa tatizo la homoni lililompa shida kwenye kukua huku makubaliano ya matibabu hayo ikiwa ni kusaini mkataba wa kujiunga na La Masia (Academy ya Barcelona) kama mchezaji wao, kwa mara anaingia timu ya wakubwa mara baada ya mkataba wake wa kwanza ambao ulisainiwa kwenye tishu kutokana na karatasi kuwa mbali alikutana na Ronaldinho Gaucho na Samweli Etoo kwenye eneo la ushambuliaji wakiwa wamotooo yeye akaingia akauwashaa, baadae kidogo akasogezwa Thierry Henry na Alexander Helb kwenye eneo hilo mwamba akaendelea kuuwaasha, kidogo akaletwa Zlatan Ibrahimović na David Villa, La purga bado akauwasha, akaletwa Alexis Sanchez na Pedro Rodriguez bado moto wa Messi ukawaka hata alipoletwa Neymer na Luis Suarez moto wa Messi ulikuwa ni ule ule nadhani hata kumbukumbu zetu za mwisho zitakuwa sawa kuwa Messi bado alikuwa katika ubora wake hata alipokuwa na kina Antonie Griezmann na Osman Dembele, ahsante Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kumuona Lionel Messi akifanya vitu vyake uwanjani.

Mwamba huyu mwenye mataji mbalimbali na tuzo nyingi zaidi za mchezaji bora wa dunia akiwa na Ballon D’Or sita mikononi mwake awali huenda alikuwa hapati heshima anayostahili kutokana na kuwepo kwenye kivuli cha ushindani dhidi ya Mreno, Cristiano Ronaldo lakini mara baada ya ndoa yake na FC Barcelona kufikia ukingoni, Messi ameanza kupata heshima anayostahili kwa ukubwa wake, FC Barcelona walimthamini Messi akiwa si kitu na leo wamewezesha kuuonesha ukubwa wake baada ya kumtema.

Kila kitu huwa kinatokea kwasababu huenda sifa hizi zinazozunguka kwenye mitandao na vyombo mbalimbali vya habari duniani kwa takribani wiki mbili sasa tusingezisikia labda mpaka siku ya kifo chake kutokana na kivuli kizito cha ushindani na Cristiano Ronaldo, Messi huyu ambaye hana muda wa kujitengeneza kama chapa iwe kimuonekano, mazungumzo, matukio na hata mtindo wa maisha angeweza vipi kufua dafu mbele ya bishoo Ronaldo zaidi ya kuwa busy kwenye kufanya yasiyowezekana na wengine ndani ya uwanja? lakini ukomo wake wa kuitumikia FC Barcelona na kujiunga na matajiri wa Ufaransa PSG umeonesha ukubwa wake na ni kwa namna gani ana ushawishi mkubwa ndani na nje ya uwanja na hilo limedhihirika wazi kwa kuziongezea kurasa za mitandao ya kijamii za PSG wafuasi maradufu mara baada ya kutangazwa kwa deal yake.

Andunje aliyefanya kila kitu kinachohusu mpira wa miguu kwenye dunia hii, Messi aliyeandika kila rekodi isiyofutika leo hii kwa kung’oka ndani ya FC Barcelona amezipata sifa zake maradufu huenda ndani ya Paris Saint German ukawa ndiyo mwisho wa kumuona Lionel Messi kwenye ubora wake akiwa kwenye soka la ushindani, usifanye bahati mbaya kusanya mizigo yako na kwa pamoja tukaitazame kwa ukaribu ligi kuu ya nchini Ufaransa na michuano ya ligi ya mabingwa barani ulaya ndani ya king’amuzi cha DStv tuweze kukishuhudi kiumbe hiki chenye talanta ya kipekee kwa sasa kikiwa na umri wa miaka 34 kikienda kumaliza soka lake.

Wakina Ronaldo, Iniesta, Neymer, Mbappe, Bruno Fernandes watatokea wengi sana lakini kutokea kiumbe kingine kama MESSI kwenye mpira huu itapita hata miaka 100, hii ni zaidi ya talanta tena yenye maajabu, tunafurahi kuona kwasasa amepata sifa anazostahili nadhani kilichobaki sasa ni heshima tu na hii ataipata kutokana na yale atakayoyafanya ndani ya PSG.

Wazee wa PlayStation na FIFA sasa hivi ni jino kwa jino, ukiwahi PSG mwenzako atachukua Paris Saint German, Ahsante sana Mwenyezi Mungu kwa kutuletea na kutuwezesha kumuona Lionel Andrés Messi tuna cha kuhadithia kwenye kizazi cha kesho…Messi Messi Messi Messiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii!!