Ngoja tufungashe mizigo yetu kwa muda tukijiandaa na safari ya kuelekea mapumzikoni baada ya mambo mengi yaliyojiri ndani ya muda mfupi nchini.

Kiukweli yaliyojiri ni mengi na yamezipa bongo zetu uzito wa kufikiri tena na tena nadhani safari hii itenda kurefresh na kurejesha upya ufikiri wa bongo zetu, niombe tu tusisahau kubeba visimbuzi vyetu vya DStv ili tuweze kufahamu na kuona yale yote yanayoendelea nchini kupitia Plus Television channel 294 ndani ya king’amuzi cha DStv kipindi chote tukiwa Accra kwasababu Plus TV inaonekana kwenye zaidi ya nchi 36 barani Afrika ikiwemo Ghana ambako ndipo tunapoelekea kwenye mapumziko yetu lakini kabla hatujafika huko tuwekane sawa kwenye mambo kadhaa.

Niliwahi kuuliza ni nini maana halisi ya upinzani na utofauti wake kwa maana ya vyama vya upinzani lakini sikupata majibu sahihi moja kwa moja, kila pahali walitoa tafsiri ya uelewa walionao na wengi walilinganisha na kile kinachoendelea kwenye mazingira yanayowazunguka. Sijui kama nikuchukua tafsiri ya upinzani wa kwenye mpira wa miguu, ndondi au mbio za magari zitaleta maana halisi ya kwenye hili la vyama vya upinzani kwa upana wake, hebu tuliache kidogo lakini siamini kwenye haya yanayoendelea nchini kwasasa kama ndiyo maana halisi ya upinzani, sometimes tunahitaji kubadilika au hata kuwa wanafiki ili tuweze kuvuka kwenye hatua fulani hasa ngumu ili tuweze kusogea kwenye unafuu.

Baada ya kufanya mambo mengi ya ujana na kuacha maumivu ya mioyo kwa mabinti, Dony aliamua kubadilika na kuingia kwenye maisha ya utulivu ili kujenga familia yake na binti mmoja aliyempatia ujauzito kwani aliona umri unakwenda na muda unazidi kuyoyoma.

Habari za jioni viongozi, marafiki na wafanyakazi wenzangu napenda kuwataarifu kuwa mwanzoni mwa mwezi ujao natarajia kuingia rasmi kwenye maisha ya ndoa” yalikuwa ni maneno ya Dony mbele ya wafanyakazi wenzake kwenye mkutano mmoja wa ofisi, wapo walioshangaa, wapo waliombeza kutokana na kufahamu uhalisia wa maisha yake ya kabla lakini ukweli ulikuwa ndiyo huo Dony aliamua kubadilika ili kujenga maisha yake.

Nani asiyefahamu yale tuliyopitia kwenye nchi yetu miaka kadhaa iliyopita, nani asiyefahamu ugumu tunaopitia sasa kutokana na changamoto ya mlipuko wa uviko 19? hatupo pazuri sana, huenda tulipotoka siyo pazuri pia sasa kwanini tusisimame kwenye eneo moja ili tuweze kuvuka kwa pamoja katika hili tunalopitia sasa? sidhani kama ni afya ya siasa viongozi wa vyama kuendelea kutukanana, kutoleana maneno ya kashfa au kukamatana kamatana tena kwenye zama hizi, inaumiza na wakati mwingine inaudhi.

Wapo wanaoamini maana halisi ya kuwa mpinzani wa mwenzako hasa kisiasa basi nikukamatwa kamatwa uonekane unaonewa, kujigamba au kumtolea maneno ya kashfa mwenzako, Ndiyo huenda wakawa wapo sahihi kutokana na tafsiri yao lakini unafanya matukio hayo kwa wakati upi?

Nimejaribu kufuatilia kwa karibu siasa za majirani zetu kwenye kipindi hiki ambacho dunia inakumbwa na janga zito la uviko 19 kwa asilimia zaidi ya 90% hakuna kama haya yanayoendelea kwetu kwasasa, sasa basi huenda wanasiasa wetu hawajui ni wakati gani wa kusogeza ajenda lengwa au magumu yamewafikia ukomo ama wanatamani tufike kwenye nchi ya ahadi mapema zaidi.

Ndiyo, Katiba mpya ni muhimu sana lakini je wakati tunaodai iundwe ni sahihi, sawa kodi za miamala ya simu ni muhimu lakini je ongezeko tuliloweka ni sahihi kwa wananchi katika kipindi hiki, upinzani wa kukimbizana, kukamatana, fujo, kutotii au kutumia mabavu ni wakati sahihi huu kuendelea kuonekana kwenye nchi yetu?.

Tupo na mambo mengi sana ya kufanya hivi sasa ili tuweze kufika kule tunapopaota lakini bado tuna vita kubwa dhidi ya adui (Uviko 19) ambaye anarudisha vitu vingi nyuma, hapo hapo tuweke siasa za upinzani wa mshike mshike, hapo hapo tutengeneze Katiba mpya, hapo hapo tuwakamue wananchi kwenye miamala, tutafika kweli?

Huenda tumepitia mengi magumu, huenda tunapopaota ni pakubwa zaidi, huenda bado tunataka kufanya mengi ya kurudisha imani kwa wananchi, kujenga vyama na kufidia kwenye yale tuliyoyakosa ndani kipindi fulani kilichopita.

Tulikosea, tulipatia, tulikwazana lakini miaka inakwenda na nchi yetu inazidi kukua, teknolojia inazidi kwenda mbele na changamoto zinakuja kwa wingi wake kama ilivyo ya Uviko 19 kwasasa, vyama vya siasa tulivyo ndani yake kwa sasa vitabaki lakini sisi tutaondoka na nchi itaendelea kuwepo. Tukae kwa kutulia, tushatengeneza ujauzito wa changamoto, maumivu, malengo makubwa n.k tutulie tuijenge nchi kwa umoja wetu, huenda tukabezwa, tukachekwa kuwa tumelainika au kununuliwa, tukubali hata kuwa wanafiki ili tuweze kuvuka kwenye hili, nadhani kwa leo inatoshea hapa, acha sisi tuelekee mapumzikoni Ghana tukazipe uhuru na upya mbongo zetu inshallah tutarejea.