Tarehe 5 ya mwezi April mwaka huu wa 2021 nilishika karamu nyekundu kwenye mkono wangu wa kushoto na karatasi nyeupe zaidi ya nne zisizo na maandishi yeyote mkono wangu wa kuume kwa ajili ya kuwapongeza kwa ujumla wake klabu ya Simba Sports Club kutokana na yale makubwa wanayoyafanya tangu wametangaza rasmi kuingia kwenye mfumo wa mabadiliko huku lengo langu kuu likiwa ni kuwashtua watani wao wa jadi, Dar Young Africans nao waige kile kilichofanywa na wenzao (kwenda kwenye mabadiliko) kwani kunaonekana kuna faida kubwa na kutalinyayua kwa kasi soka letu na andiko hilo nililipa jina la ‘Yanga wana cha kujifunza kwa watani’.

Nikiwa katikati ya uendelevu wa maandalizi ya kuandika andiko langu hilo kwa karatasi kadhaa, ghafla nilijikuta nakomea njiani kwa nguvu kutokana na kile nilichokiona kupitia kipindi cha Sports Bomba cha Plus Television na Ester Maongezi, Wilson Oruma na Gwamaka Francis kinachoruka kila siku za wiki kuanzia saa 2:30 za usiku kupitia king’amuzi cha DStv channel namba 294, ilikuwa ni press conference ya Msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara na waandishi wa habari na nilikomea njiani kuandika andiko langu kutokana na majibu aliyokuwa akiyatoa msemaji wa klabu hiyo pindi alipokuwa akiulizwa maswali na waandishi.

Si kwamba yalikuwa majibu mabaya lahasha! bali yalikuwa si ya kujibiwa na msemaji wa klabu tena klabu kubwa kama Simba, kwa upande wangu niliona anayejibu yale maswali ni Haji Sunday Manara (shabiki wa Simba) na si Haji Sunday Manara (Msemaji wa klabu ya Simba) nikajisemea moyoni ngoja nijipe muda kuandika andiko langu lisije kuniumbua mbele ya safari kwani haya mabadiliko nayoyafikiria na vitu nilivyoanza kuviona kwenye klabu ya Simba, si kwa hivi Msemaji wa klabu kutoa majibu yenye ukakasi kwenye hadhira tena hadhira ya waandishi wa habari, Yanga wataiga nini kwenye hili kama navyotamani iwe. Siku zikasonga na hapo taratibu nikaanza kupunguza karatasi moja moja kwenye andiko langu kutokana na vile vilivyokuwa vikiendelea ndani ya klabu hiyo, kulionekana kabisa kuna wingu zito lililotanda hasa kwenye uongozi, utoaji wa taarifa haukuwa sawia tena, Msemaji kasema hili, CEO kasema lile na kiongozi yule kasema hilo lakini jambo ni hilo hilo moja ambalo lilihitaji utulivu mdogo wa kuja na taarifa moja tu kama klabu ambapo utaratibu huu ulifanya kazi sana chini ya aliyekuwa C.E.O Mr.Senzo ambaye kwasasa anafanya kazi zake upande wa Dar Young Africans na yeye wakati anatimka Simba alisema wazi kuwa kwenye uongozi wa klabu hiyo kuna hitilafu hivyo ingekuwa ni ngumu yeye kutimiza majukumu yake kwa usahihi kama angeendelea kusalia klabuni hapo.

Simba hii inayoogelea kwenye mfumo mpya wa mabadiliko na kama ambavyo watu wengi wasemavyo kuwa Simba kwa sasa imekuwa kubwa na imejitahidi kuonesha ukubwa huo kila uchao lakini imeonekana kuwa na changamoto kubwa ya kutokuwa na watu sahihi kwenye nafasi mbalimbali hasa za uongozi, tusifukue makaburi sana maana hatutafikia ukomo kwenye hili kwasababu yapo mengi mengi mno ambayo yanaonesha licha ya kuwa kwenye njia ya kukua kama klabu lakini wana hitilafu ya kukosa watu sahihi kwenye uongozi (utendaji) na hili limeanza kujidhihirisha wazi kwenye sintofahamu inayoendelea kati ya Msemaji wa klabu hiyo Haji Manara na C.E.O wa klabu hiyo Barbara Gonzalez, ingawa mpaka sasa umesikika mubashara upande mmoja tu wa Haji ndiyo unaopeleka shutuma za wazi kwa Barbara na hapo ndipo unapojiuliza kwa maneno yanayosikika kwenye voice note inayotembea kwenye mitandao ya kijamii ya Haji akitoa shutuma zake kwa Barbara ni kweli Haji alipaswa kuwepo kwenye nafasi ya utendaji wa klabu ya Simba hasa kwenye Simba hii ya mabadiliko tena wakiwa wanaelekea kwenye mchezo mkubwa dhidi ya watani zao? Na je, yale yanayoshutumiwa na Haji kwenda kwa Barbara kupitia voice note ile kama ni ya kweli, Barbara alipaswa kukaa kwenye kiti cha C.E.O wa Simba hasa hii iliyopo kwenye mabadiliko? maneno yamekuwa ni mengi mno lakini nafikiri sasa mvua imeanza kunyesha na acha inyeshe ili tuone panapo vuja.

Tatizo kubwa lililopo ni kuwa Haji ana kofia nyingi na kwa kiasi kikubwa amekuwa akishindwa kuzitofautisha kofia hizo hata kwenye utendaji wake, Haji Msemaji wa klabu, Haji Influence na Mfanyabiashara, Haji Shabiki wa Simba, kofia hizi zimekuwa hazina utofauti kwa Haji na sasa imepelekea Haji kuonekana ni mkubwa kuliko klabu na viongozi wa Simba wamekuwa kimya muda wote na mwisho yamefikia hapa (ya kama ni kweli tofauti zake na Barbara) ambavyo kimsingi ilibidi vitu hivi viwe binafsi leo vimekuja kuichafua chapa ya Simba na kuwavuruga mashabiki kuelekea mchezo mkubwa wa Derby dhidi ya watani wao.

Hebu tujiulize maswali kadhaa kwenye sakata hili la Haji Manara dhidi ya Barbara Gonzalez, Je Manara kama Afisa wa habari wa klabu alishindwa kuyafikisha malalamiko yake na sintofahamu dhidi ya Barbara kwenye uongozi wa juu?,  Manara ameshindwa kuvumulia haya kwa muda mfupi kuupisha mchezo wao dhidi ya Young Africans ndipo aanze kutangaza habari za magumu anayoyapitia ndani ya Simba na kung’oka kwenye klabu kuepusha sintofahamu kwa mashabiki, wachezaji na uongozi na kama ni kweli anataka kung’oka Simba kwanini aanze kusema mambo ya ndani kana kwamba kuiomba huruma kwa watu, kwanini asing’oke kimya kimya?

Na kama yanayosemwa na Manara kwenda kwa Barbara yana ukweli, Barbara kama mkuu wa waajiriwa wote ndani ya Simba akiwemo Manara alishindwa kuyamaliza haya na Manara ili awapishe klabuni kama ni kweli alikuwa hatoshi, kwanini amtishe? kwa ukubwa wa Haji na kazi aliyoifanya kwa kipindi chote ndani ya Simba ni kweli alipashwa kulipwa kiasi kile alichokisema na kufanyiwa haya anayofanyiwa sasa (kushutumiwa)? na Barbara kama kiongozi kwanini hataki kushaurika?

Zote hizi ni shutuma na bado hazijathibitishwa ukweli wake lakini kiukweli Simba hasa uongozi wa juu inabidi wajitafakari sana kwenye kuwaweka watu sahihi kwenye nafasi za uongozi wa klabu hasa kipindi hiki cha mabadiliko, wanaweza wakanunua wachezaji wazuri, wakajenga miundombinu mizuri lakini kama hawana uongozi thabiti basi ni kazi bure, Mzee Mpili ana watu, Yanga ina wana watu, kama wakipoteza tena kigoma wasitafute mchawi nani tatizo limeanzia hapo wakae chini na wajiulize mabadiliko yao yana watu sahihi?