Ilani Ilani Ilani, “hakuna mwenye wasiwasi juu ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwasababu tunaongozwa na ilani ya chama cha mapinduzi ambayo nae alikuwa ni mmoja wa walioitengeneza” hii imekuwa ni miongoni mwa kauli kuu wanayoitumia wanachama mbalimbali wa chama cha mapinduzi ikiwemo wabunge kwenye kuweka msawazo wa sintofahamu pindi vilima vya yasiyokuwa sawa vikisimama.

Kitu kikubwa ambacho kinaweza kuwa ni ushindi mkubwa wa chama cha Mapinduzi na wanapaswa kujivunia ni namna ambavyo wanachama wake wamekuwa wakiibuka na kujibu hoja ya yale yanayoonekana si sawa au yanahitaji maelezo zaidi iwe ni kuhusu serikali au chama, kwenye hili tunaweza kusema CCM ina watu lakini moja ya vitu vinavyowachanganya wengi ni utofauti wa majibu ya hoja au maelezo ya jambo fulani kuwahusu wao na serikali pindi wanapojitokeza wanachama wao kuzungumza.

Hapo ndipo wengi hujiuliza je, ni kweli wanachama wote wapo kwenye mstari mmoja, Je ni kweli wanaijua na kuifuata ilani kama wanavyoitumia kwenye kuweka msawazo pindi vilima vya yasiyo sawa vikisimama?. Huyu atajibu A, yule atatoa maelezo B na wale watajieleza C hapo ndipo utakapojiuliza tena hawa wameisoma kweli ilani yao au wanauza nayo sura kwa kuibana kwapani kama kipima joto pindi wakitembea? Hapo ndipo pakubwa wanapotuachia maswali, anyway ngoja tuliache hili kwa sasa na turudi kwenye pointi ya msingi huenda huu ni utaratibu wao tu.

Moja ya mjadala mkubwa unaoendelea kwa sasa kwenye mitandao ya kijamii na maeneo mbalimbali nchini ni juu ya tozo mpya za miamala ya simu ambazo zimepitishwa kwenye Bunge la bajeti la mwaka 2021/2022, Bunge ambalo wabunge wake zaidi ya 250 wanatoka chama cha mapinduzi lakini kitu cha kushangaza kidogo ni utofauti wa maelezo au majibu ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya wabunge wa CCM juu ya tozo hizi mpya jambo ambalo limeendelea kuleta sintofahamu kwa wananchi ambao wengi wao wanaamini wangepata majibu sahihi kutoka kwao kwani wabunge hawa wote wapo kwenye mwamvuli wa ilani moja na ndiyo waliolipitisha hili kwa kishindo.

Kwakuwa kuna utofauti wa maelezo na hakuna usahihi wa moja kwa moja wenye kuleta uelewa hapo ndipo kumezidi kuleta manung’uniko kwa wananchi ambao wengi wao huenda hawajui hata namna ambavyo tozo hizo zinakatwa na kama ni kweli zinawakandamiza au laah!, kwa kuwa wengi wanalalamika na yeye anaunga humo humo tena ukizingatia wametoka kwenye wakati wa vyuma kukaza (uchumi mgumu) kipindi cha serikali ya awamu ya tano basi ataegemea wanapolalia wengi kila anapopata nafasi.

Kwenye hili pia wapo wabunge wa vyama vya upinzani ambao nao wana ajenda zao nyingi wanazotaka kuzipa nguvu wakati huu hivyo serikali inaposhindwa kufikisha vitu kadhaa kwa usahihi kwa wananchi basi wao wanapita na njia hiyo hiyo ili wapate nafasi kusogeza ajenda zao kuu kwa urahisi ambazo kiukweli wakati wa serikali ya awamu ya tano ilikuwa ni ngumu kidogo kuzisogeza (na hiyo ndiyo siasa).

Laiti kama tungekuwa na katiba mpya au tungeruhusiwa kufanya mikutano ya kisiasa basi tusingekuwa na tozo kama hizi” – Penye uzia, penyeza rupia

Iliwahi kutokea sintofahamu kama hii kwenye bei ya vifurushi vya simu miezi kadhaa iliyopita wananchi wakapaza sauti na kweli serikali ikalisikia na kulifanyia kazi, ni sawa kwenye lile la vifurushi ilikuwa ni kuteleza kwa wizara husika, makampuni ya simu labda na TCRA lakini hili la tozo limepitishwa na wawakilishi wetu pale bungeni tena wapo kwenye mwamvuli wa ilani moja kwanini washindwe kutupa maelezo sawa sawa yatakayotufuta ukungu wananchi?

Wananchi wanajua Mama ni msikivu kwahivyo kwenye lolote lile watakaloona haliko sahihi kwa upande wao watapaza sauti (tunadeka sana), lakini je ni kweli hili la miamala linaumiza kama wengi wetu tulalamikavyo tofauti na wawakilishi wetu ambao wamekuwa wakipishana maelezo na wengine wamekuwa wakijigamba kabisa kuwa wamepitisha hili na lina faida hivyo ni lazima wananchi tulikubali?, kwanini wasitupe maelezo sahihi na sisi tusimame kwenye uelewa kama waliousimamia wao kwa sasa kuwa ni wa faida?

Waziri wa fedha na mipango pekee hawezi kulimaliza hili, wakae serikali, wadau na wabunge waone faida ni zipi na hasara ni zipi kwenye hili na ni kwa namna gani wanaweza kutoa elimu kuanzia majimboni ili wananchi wapate elimu sahihi ya jambo hili.

Tusiwape wananchi sintofahamu na kuwaumiza kiuchumi katika hili kwa maana kwenye hili la tozo za miamala tuna watu, tena tuna watu wa hali ya chini ambao ndiyo wanaguswa na hili moja kwa moja.