Mambo za business, mambo za biashara, heri ya siku ya wafanyabiashara sabasaba day popote pale ulipo, kama unafanya biashara au unahusika kwenye biashara kwa namna yeyote ile basi simama na ugonge upande wako wa kuume wa kifua chako mara saba kwani upo sehemu salama. Biashara huwa haidanganyi wala kukuongopea kwa namna yeyote ile kama unajituma, unafuata utaratibu, unakuwa mkweli au kutumia uongo usio na madhara pamoja na kumingo vizuri na wateja wako basi utafanikiwa tu endapo pasipotokea changamoto za hapa na pale.

Utamu mwingine uliopo kwenye biashara ni kuwa kifursa utawagusa wengine kwa namna moja ama nyingine hivyo utaisaidia nchi kwenye suala zima la kupunguza uhaba wa ajira. Kwa kuanzia acha kwanza nipeleke pongezi zangu za dhati kwa mwanamke shujaa, Zamaradi Mketema kutokana na kile nilichokikuta pale viwanja vya maonyesho ya sabasaba na hii ikiwa ni kwa mwaka wa pili mfululizo kutokana na kazi kubwa anayoifanya mwanamke huyu shujaa bila kusita.

Kwa kipindi kirefu wadau mbalimbali wa sanaa nchini wamekuwa wakipiga kelele na kutamani kuwaona wasanii wakifungua milango ya kutumia chapa zao kwenye kufanya biashara nje na muziki, marehemu Ruge Mutahaba alilipigania hili pia kwa nguvu zote katika kuhakikisha wasanii wanazisimamisha chapa zao katika kutengeneza fedha kwa biashara.

Umekuwa ni mjadala usiokauka kila nikitazama kipindi cha On Air cha Plus Television channel namba 294 kwenye king’amuzi changu cha DStv ambapo kwa shilingi 19,900 tu ya kifurushi cha DStv Bomba huwa inaniwezesha kuburudika mwezi mzima kwa kupata channel mbalimbali. ‘Wasanii ni lini wataanza kutengeneza pesa za kibiashara kupitia chapa zao?, Wasanii wanazitumia vipi chapa zao katika kufanya biashara nje ya muziki?’ najaribu kunukuu sentensi za Mwanadada Lesa Sid akiwa anazitambulisha baadhi ya mada hizi zihusianazo na wasanii kwenye On Air.

Hata ukirudisha kumbukumbu zako hadi Jumanne ya Juni 15, 2021 wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan akizungumza na vijana jijini Mwanza alionyesha tamaa yake ya wazi ya kuona wasanii wakitengeneza fedha kupitia kazi zao na hata chapa zao na leo hii Zamaradi amekuja kulitimiza hili. Ukitembelea kwenye viwanja vya sabasaba kwa sasa utakutana na mabanda maalumu ya wasanii na watu maarufu wakiwa na bidhaa zao mbalimbali ambapo wao wenyewe ndiyo wanakuhudumia, ni nani atakayeshindwa kwenda kununua bidhaa hata kama ni pipi kwa mtu anayemuhusudu? kupitia jukwaa hili nadhani unaweza ukawa mwanzo mpya kwa wasanii wetu kuona ni kwa namna gani wanaweza kuzitumia chapa zao kwenye kufanya biashara na huenda wakapata mafanikio makubwa tofauti na hata yale wanayoyafikiria kwenye muziki.

Zamaradi ameanza kubeba ushindi wa kile alichokuwa akikipigania Marehemu Ruge, Zamaradi amesogeza ubingwa wa kile walichokuwa wakikiota wadau mbalimbali wa sanaa, Zamaradi amepeleka ushindi wa kile anachokitamani Rais Samia kutokea kwa wasanii wetu, Kwenye hili Zamaradi amekuwa na damu ya kiitaliano kama vile ya wachezaji wa Azzuri na wanachokitaka kukifanya kwenye Euro 2020.

Gianluca Vialli na Robert Mancini

Kwenye Benchi la ufundi la timu ya taifa ya Italia chini ya Roberto Mancini yupo msaidizi wake Gianluca Vialli ambaye kwa sasa anasumbuliwa na saratani ya kongosho ambayo muda wowote huenda ikamuondoa (ikamuua) kwa mujibu wa madktari. Vialli aliachana rasmi na mambo ya soka mwaka 2000 kama kocha baada ya kuanza kupata changamoto kwenye afya yake lakini mwaka 2021 aliamua kujiunga na kikosi cha timu ya taifa kama msaidizi wa Mancini.

 Kabla ya kuanza safari ya michuano ya Euro 2020, Vialli aliwaambia wachezaji wa Italy kuwa “hali yangu ya kiafya si nzuri na muda wowote kuanzia sasa huenda nisiwepo kwenye uso wa dunia, naomba mpambane na mnipe ubingwa wa Euro 2020 kama zawadi yangu kabla sijafariki”. Wanaume wakalibeba hilo wakaenda nalo kwenye Euro wakaanza kupambana kwa jasho na damu kuhakikisha wanampa Vialli kile anachokiota. Wakiwa katikati ya mashindano ghafla mchezaji mwenzao Leonardo Spinazzola akaumia hivyo ikabidi aondolewe kikosini na kurudishwa nyumbani Rome kupata matibabu ambapo huko huko Rome, Baba Mtakatifu Francisco naye yupo hospitalini akipata matibabu kutokana na kupata changamoto za kiafya, wanaume damu ikawaka, wamezidi kuwa wamoto sasa hawapiganii tu ndoto ya Vialli bali wanataka kupeleka ndoo kwa mwanajeshi mwenzao Spinazzola aliyeumia katikati ya vita na kwa Baba Mtakatifu ambaye kwa sasa anapitia changamoto ya kiafya ili wapate hata moshi wa chetezo kutoka kwenye mikono yake.

Zamaradi amesimama kupigania kile alichokiota Ruge, wadau na Rais Samia, wachezaji wa Italia nao wamesimama kuhakikisha wanapigania kile anachokiota Vialli, Spinazzola, Baba Mtakatifu na waitalia kwa ujumla…..hiyo ndiyo damu ya kiitaliano, kutii na kufanya maagizo ya wanachokiota, Zamaradi na Wachezaji wa Italy sasa hivi utawaambia nini (kwa sauti ya Prof.Jay) zaidi ya kubeba ndoo? tuendelee kuangalia mwisho wa damu ya kiitaliano.