Juni 15, 2021 huenda ikawa ni miongoni mwa siku kubwa za kukumbukwa kwa vijana wa Tanzania hasa wa jiji la Mwanza ambapo kwa wingi wao walipata nafasi ya kuzungumza na Rais wa awamu ya sita wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan.

Hii huenda ilikuwa ni fursa pekee ya vijana kufahamu ni kwa namna gani wana nafasi kubwa kwenye kuijenga nchi kwa sasa ambapo Rais Samia aliweka wazi namna ambavyo serikali yake itatoa nafasi kubwa kwa vijana, kongole kwa vijana kwa heshima na umuhimu mkubwa walioonyeshwa ‘The Future Is Bright’ yajayo hayapimiki kwa kweli, wazee wamepewa dira, wakina Mama wamepewa dira, Vijana wamepewa dira, vipi watoto?

Juni 16 kila mwaka bara la Afrika huazimisha siku ya mtoto wa Afrika ‘International Day of the African Child’ ambapo kikubwa huwa ni kuangazia haki, namna ya kuwalinda, kuwatunza na kuwalea watoto wetu tukiwa tunawakumbuka watoto wa Soweto kule Afrika ya Kusini ambapo mwaka 1976 walisimama kidete kwenye kupigania haki ya kupata elimu bora kwa watoto weusi.

Ukarimu unaanzia nyumbani, Mwaka 2013 tulifunga safari kwenda kutazama maendeleo ya ujenzi wa miongoni mwa majengo marefu barani Afrika kwa sasa ‘Jengo la Mamlaka ya Bandari Tanzania’ TPA ambao umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 140 likiwa na urefu wa Mita 157 lakini wataalamu wanasema ukirudi nyuma kidogo rekodi inaonyesha kuwa majengo mawili ya PSSSF yaliyopo Posta jijini Dar es Salaam ndiyo yalikuwa majengo marefu zaidi nchini na Afrika Mashariki yakiwa na urefu wa Mita 153 lakini miaka ikasonga, utaalamu na teknolojia ikaongezeka zaidi hivyo wajenzi wakaja na Jengo refu zaidi la TPA kuliko la awali la PSSSF ambapo ukitazama rekodi, jengo la TPA linasimama kwenye nafasi ya 9 ya majengo marefu zaidi Afrika nyuma ya Leonardo na Carlton yote ya Afrika Kusini, Britam la Kenya, CBE Headquarter la Ethiopia, Nairobi GTC la Kenya, Ponte City la Afrika Kusini, UAP Tower la Kenya na Necom House la Nigeria, hii inaonyesha wazi kuwa teknolojia na utaalamu unazidi kuongezeka kadri siku zinavyosonga na huenda baada ya miaka 10 orodha hii ya majengo marefu barani Afrika ikabadilika, yaani yakajengwa majengo mengine marefu zaidi ya haya.

Miaka inakwenda utaalamu na ujuzi unaongezeka leo tukiwa tunaadhimisha siku ya mtoto wa Afrika unamuandaaje kijana wako kuishi sawa na mabadiliko hayo ya teknolojia mbeleni?

Ukirudi kwenye historia hadi zama za mawe za kale inaonyesha dhahiri kuwa mwanadamu alihitaji nguvu zaidi kuliko chochote ili aweze kuishi jambo ambalo ni tofauti kidogo na sasa na hii ilienda hadi wakati wa biashara ya utumwa ambapo mataifa mbalimbali ya ulaya yalikuja barani Afrika kwa ajili ya kuwapata watu wenye ubavu ili iwe nguvu kazi yao kwenye mambo mbalimbali lakini baadae zikagundulika mashine na viwanda hivyo nguvu za watu zikawa hazihitajiki kwa kiasi kikubwa sana zaidi ya maarifa.

Kufupisha habari tunaweza kusema tumetoka kwenye zama za nguvu na sasa tupo kwenye zama za maarifa, inabidi uwe na vyote hivi viwili ila maarifa zaidi ili uweze kuishi, umempangaje kijana wako kwa zama zijazo ambazo ni zama za……….

Tujifunze kwa waliofanikiwa, kama una chenji chenji kidogo kata tiketi zako mbili twende kwa waliofanikiwa tukajifunze, tiketi moja iwe ni ya Marekani na tiketi ya pili iwe ya pale Ureno, kama hauna chenji za kutosha basi lipia shilingi 19,000 tu ya kifurushi cha DStv Bomba then press channel 294, Plus TV utazame Sports Bomba na Gwamaka Francis nadhani atatusafirisha kiurahisi kwenye safari hizi.

Twende mpaka maandishi matatu U.S.A pale Florida, Palm Beach Gardens kwenye mjengo wa mcheza tennis nguli duniani Serena Williams halafu uone anafanya nini na binti yake Olympia Ohanian nyuma ya nyumba yao, ni tizi kali la kufua wepesi wa mikono na utimamu wa mwili, hela anayo, mtoto anasoma pazuri lakini bado anampa tizi la kunoa kipaji chake.

Twenzao twenzetu hadi pale Brentwood, Los Angeles kwenye mjengo wa nyota wa kikapu duniani Lebron James mtazame anafanya nini na kijana wake Bronny James kwenye court pembeni ya nyumba yao, ni jasho tu inamwagika kunoa mikimbio na mitupo kwenye kikapu, hela ipo, maisha A+, pa kusoma pazuri lakini tizi la kukuza kipaji linaendelea kwa Bronny.

Tumalizie safari yetu pale Madeira Ureno, huku tukae kwa mbali kidogo tusije tukapatwa na huruma na kile kinachomtokea mtoto kwenye mjengo wa Cristiano Ronaldo akiwa na kijana wake Cristiano Junior, mazoezi makali na usimamizi wa ng’adu kwa ng’adu ndiyo unaomkuta Cristiano JR kila asubuhi, pesa ipo, nyumba ipo na anasoma pazuri lakini bado mshua anamkomalia kukinoa kipaji chake na matokeo ya tizi hili nenda pale Juventus Academy utapewa habari za Cristiano JR.

Kwanini tumewaangalia hawa? Leo tunaadhimisha siku ya mtoto wa Afrika ambapo chimbuko lake lilikuwa ni vifo vya mashujaa waliokuwa wakipigania haki zao za kimsingi za elimu kwa watoto weusi na hatimaye leo hii ikapatikana mifumo bora ya elimu, ukirudi nyuma kidogo hapo tulisema kuwa tumetoka kwenye zama za manguvu, tukafika kwenye zama za maarifa na sasa tunaelekea kwenye zama za vipaji, teknolojia inakuwa na mambo yanabadilika kama ilivyokuwa kwenye rekodi ya maghorofa marefu kesho utaalamu utakuwa mwingi zaidi huenda usihitaje maarifa pekee.

Cristiano, Lebron, Selena na wengine wengi huenda wameshanusa hiki, tunaelekea kwenye mapinduzi ya kiteknolojia kwa ukubwa wake, elimu pekee huenda isimfanye mtu aishi kwa ufasaha kama ilivyokuwa kwenye zama za maarifa dhidi ya nguvu, leo tunapoadhimisha siku ya mtoto wa Afrika mzazi na mlezi hakikisha unaijenga kesho ya kijana wako, nguvu na maarifa pekee hayatamfanya aishi kwa fasaha uko tuendako bali ni nguvu, maarifa jumlisha kipaji.

Wenye nguvu watakuwa wengi, wenye degree na PHD za…..watakuwa wengi lakini vipaji hata vikiwa vingi havitalingana hata kidogo, akishindwa kubeba mzigo ataletwa mwenye nguvu mwingine abebe, akishindwa majukumu kwenye eneo fulani alaletwa mwenye elimu sawa na yake kuchukua nafasi lakini aking’oka kwenye kipaji chake hakuna wa kukiziba sawa na yeye, kipaji ni kipaji huwa hakuna mfanano.

Michezo ni biashara kubwa, muziki ni biashara kubwa, sanaa kwa upana wake ni biashara kubwa zinazokuja kwenye zama za vipaji, ili uweze kuishi na kutengeneza fedha nyingi kwenye zama hizi ni lazima uwe na nguvu, maarifa na kipaji.

Mpe malazi, mpe makazi, mpe chakula mtoto apate nguvu, mpeleke shule apate maarifa lakini mkomalie apate pakukuza na kulea kipaji chake kwa ajili ya kesho, siku ya mtoto wa Afrika tuwalee watoto kimkakati tunaenda kwenye kesho ya nguvu, maarifa na kipaji hakuna fedha bila kitu cha ziada.