“Miaka kadhaa nyuma wakati mwanaharakati na mtafiti, OJ akifanya moja ya harakati zake za utafiti kwenye eneo moja jijini Dar es Salaam alichanganya karibu aina ya vinywaji vyote vilivyopo nchini na kuvitumia kwa wakati mmoja lakini kwa bahati nzuri hakivuleta matokeo hasi kama wengi walivyofikiria na mwisho wa siku akawa Man Of The Match wa utafiti ule”

Lucky You, OJ siyo kwamba life yako iko simple sana, Mungu aliweka mkono wake ili utafiti wako ukamilike ijapokuwa si utafiti sawa.

Ilimchukua miezi kadhaa Mzee Simwinga pale jijini Mbeya kukubali kipaji cha kijana wake Emmanuel ‘Izzo Bizness’ na kwa mara ya kwanza akafungua kinywa chake na kumpongeza mtoto wake huku akimtaka aongeze juhudi licha ya mkwara na msisitizo mwingi wa awali ambapo alimtaka asome na aachane na mambo ya muziki, shukrani kwa marehemu Fredwaa ambaye ndiye alikuwa mtu wa kwanza kupiga kazi ya Izzo, redioni na kumfungulia njia ya sapoti kuanzia nyumbani (kwa wazazi) hadi kwenye mainstream, leo yupo pale On Air ya Plus TV channel namba 294 kwenye king’amuzi cha DStv na muokota CD kwenye pipa ya kuhifadhia uchafu, Jimmy Jamal.

‘Kwanini hawapati nafasi na CD zao zinatupwa’? lilikuwa ni swali linalokita kwenye kichwa cha Jimmy wakati yupo kwenye kituo kimoja cha radio kama mtu wa IT kila alipokuwa akiona CD za wasanii tofauti tofauti wachanga waliopeleka kazi zao kwenye kituo hicho cha radio zikitupwa, ndipo alipojivika jukumu la kuzikusanya na kuanza kuzisikiliza moja moja na mwisho wa siku akaamini wasanii hao wanahitaji nafasi jambo lililompelekea kuhamia kwenye tasnia ya utangazaji ili awe daraja lao.

Lucky You Izzo Bizzness, Lucky You Jimmy Jamal si kwamba life yenu iko simple sana ila Mungu aliweka mkono wake amkae pale panapowagusa watu wengi.

Akiwa ameshakata tamaa ya kuendelea zaidi na masomo, Mwanadada Destiny James akiwa hana hili wala lile mwaka 2018 mara paap akadondokewa na scholarship ya takribani milioni 116 kwa faranga za Mama Samia Suluhu Hassan mubashara kutoka kwa Champagnepapi ‘Drake’ kupitia video ya ‘God’s Plan’ fedha ambazo hivi karibuni zimemuzesha kuhitimu shahada ya uzamili wa Afya katika Umma, hali iliyompa matumaini na nguvu kubwa Drake ya kuamini kuwa msaada wake ulifika pahali sahihi kama ambavyo wengi tunaamini leo hii huwa anajifungia ndani na kuisikiliza vyema Diss track ya Pusha T ya ‘The Story Of Adinon’ ambayo ilimuibua kijana wake ‘Adonis Aubrey’ ambaye alikuwa akimficha lakini leo hii anasimama kifua mbele akijivunia mtoto wake na anaamini Pusha T alimgusa sehemu sahihi licha ya kuwa alimtingisha kidogo.

Lucky You, Destiny, Lucky You Adinon si kwamba ni wazuri sana Mungu aliwatumia Drake na Pusha T kama ngazi ya kuwaweka sehemu sahihi na mnayostahili ili mje kuwagusa wengine.

Akiwa anapepea kwenye midfield ya Bolton Wenders kwenye mchezo dhidi ya Tottenham Hotspurs mwaka 2012, akiwazima na kuwaweka mfukoni vyema watoto wakiingereza wakiongozwa na Scott Parker, Kiungo Fabrice Muamba anadondoka akiwa uwanjani na moyo wake unasimama kwa takribani saa 1 na dakika 18 lakini baadae moyo ukaanza kufanya kazi tena na mwanaume huyu akawa mzima, Mwaka 2019 Mholanzi mwenye mguu wa dhahabu, Daley Blind alidondoka uwanjani kwenye mchezo dhidi ya Valencia pia mwaka 2020 kwenye mchezo dhidi ya Hertha Berlin na akaonekana ana tatizo kwenye moyo wake kiasi kilichopelekea kuwekewa kifaa maalum cha umeme chenye kusaidia moyo wake kufanya kazi kwa ufanisi, mwanaume akasimama hadi leo yupo mzima, tukio kama hili pia lilitokea juzi kwenye mchezo wa Euro 2020 uliozikutanisha timu za Denmark na Finland ambapo kiungo wa Denmark, Christian Eriksen alidondoka uwanjani jambo lililowashtua watu wengi lakini baadae akasimama tena.

Lucky You Fabrice Muamba, Lucky You Daley Blind, Lucky You Christian Eriksen siyo kwamba life yenu si special sana na mna miadi na Mwenyezi Mungu, matukio kama ya kwenu lilitokea pia kwa Marc Vivien Foe na bahati mbaya kwake hakusimama tena, Mungu amewasimamisha tena muwe mabalozi wazuri kwa wengine na uwazi wa kuwa tukumbuke kuishi lakini tunakufa mara moja tu.

Tupo hapo wenye uwezo wa kulipa shilingi 19,000 ya kifurushi cha DStv Bomba na kuitazama Plus Television kila mwezi, tupo hapo tunaopata mia mbili, mia tatu za kula tungi kila wikiendi, tupo hapo vijana wetu wanapata elimu nzuri, wanakula vizuri na kulala pazuri, tupo hapo ambao kiukweli kabisa hata kama hatuna fedha nyingi lakini maisha yetu yana utofauti na muuza muhogo wa pale Riverside ambaye usiku anajisitiri chini ya Daraja la Kijazi Ubungo.

Lucky You, mwenye uwezo wa kulipia Tsh.19,900 ya DStv Bomba kila mwezi, Lucky You mla tungi kila wikiendi, Lucky You ambaye usiku unajua unalala wapi, wewe siyo mzuri sana au life yako ni simple Mungu amekuweka hapo ili uwaguse wengi na usipotee, huenda Mungu angekuacha kabisa basi tungeona mengi na tungewapoteza wengi.

Lucky You, waguse wengi na kila mwisho wa mwezi mrudushie Mungu Zaka (fungu la kumi) kama shukrani ili mwisho wa siku uwe Man Of The Match kwenye eneo lako kama OJ.