Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo Ijumaa ya April 30, 2021 kinatarajia kufanya Mkutano Mkuu maalumu wa chama hicho kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma.

Mkutano huo maalumu utakaowahusisha wajumbe kutoka mikoa mbalimbali utakuwa na kazi kubwa moja ya kumchagua Mwenyekiti mpya wa chama ambaye atachukua nafasi ya aliyekuwa Mwenyekiti na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt John Pombe Magufuli aliyefariki dunia kutokana na matatizo ya moyo.

Mpaka sasa jina pekee lililopitishwa na Halmashauri kuu ya chama hicho kuwania nafasi ya uenyekiti ni la Mama Samia Suluhu Hassan ambaye ni rais wa awamu ya sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo wajumbe leo watakuwa na kazi ya moja tu ya kupiga kura za ndiyo au hapana.

Aidha, kwenye mkutano huo pia Katibu Mkuu mpya wa chama akichukua nafasi ya Ndugu Bashiru Ally ambaye aliteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atatangazwa.

Ni nini kitaenda kutokea leo na nani na nani watachukua nafasi za Mwenyekiti na katibu mkuu wa chama, je ipi ni dira ya CCM kutokea hapa? usikose kutazama mubashara kila kitakachojiri kwenye mkutano huo moja kwa moja kupitia Plus Television channel namba 294 kwenye king’amuzi cha DStv kuanzia saa 3 kamili za asubuhi.