Karibu sana bandugu hapa ndipo nyumbani chukua kiti uketi ama karibu jamvini nikupe mipango.. “kama una roho ndogo na nyepesi tafadhali tafuta usaidizi wakati nikikupitisha kwenye stori hii”

Haya yalikuwa ni maneno ya rafiki yangu Mzee Gogoki Kigo wakati nikiwasili nyumbani kwake nilipokwenda kwa ajili ya mazungumzo mafupi ya hapa na pale ikiwemo kwenda kusikiliza simulizi ambayo kwa kipindi kirefu amekuwa akinisisitiza tukutane ili aweze kunihadithia, sikujua ni kwanini Mzee Gogoki alitaka anipe habari hii tukiwa wawili tu tofauti na nilivyomzoea/nimjuavyo kwani mara zote alikuwa akitumwagia stori za aina yeyote ile tukiwa kwenye kijiwe chetu cha kahawa, kwa ufupi yeye ndiye alikuwa mchangamsha kijiwe.

Basi nikajiandaa vizuri na kwa utulivu mkubwa ili niweze kupata habari hizi…..kabla hatujaendelea nikuulize vipi wewe mwenzangu tayari una kisimbuzi chako cha DStv? Kama bado basi unapitwa na mengi sana kupitia channel 294 Plus TV, kamata kisimbuzi chako sasa na ulipie kifurushi cha Bomba kwa gharama ya shilingi 19,900 tu ili uweze kufaidi utamu wa burudani, elimu na taarifa zinazowasilishwa kwako kwa ueledi mkubwa kupitia Plus TV.

Tuendelee,…..Baada ya kukaa na kutega masikio yangu kwa umakini mkubwa, Mzee Gogoki akaanza kwa kusema, “Asee maisha yanaenda kasi sana na mambo yanabadilika kadri muda unavyosonga, watu wanazaliwa, watu wanafariki, watu wanaanza safari, watu wanamaliza safari, hivi vilivyotokea siku za hivi karibuni vimenishtua na kunishangaza sana”.

Akaendelea, “baada ya takribani miaka 44 ya klabu ya Manchester City ya nchini uingereza kukaa bila mafanikio ya kutwaa taji la ligi kuu nchini humo wakati majirani zao Manchester United wakiendelea kufanya mengi makubwa ikiwemo kushinda vikombe mbalimbali barani Ulaya, City waliamua kukata shauri na kufanya uwekezaji mkubwa wa kusajili wachezaji nyota wenye viwango vikubwa vya dunia ili waweze kumaliza ukame wa mataji, tunaweza kusema ni kama walidondokea kwenye sera ya Galacticos ambayo hufanywa na klabu ya Real Madrid ya nchini Uhispania.

Miongoni mwa nyota waliosajiliwa kwenye project hiyo alikuwa ni mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina, Sergio Kun Aguero aliyekuwa akikitifua kwenye klabu ya Atletico De Madrid chini ya kocha Quique Sánchez Flores ambaye kwa sasa ni Mkufunzi wa klabu ya Watford, Mwanaume aliyetitia kila alipoweka miguu yake chini na kuwapa wakati mgumu walinzi wa timu pinzani kumuweka chini pindi alipokuwa akienda kumsalimia mlinda mlango, kaangalie marudio ya mechi ya Oktoba 23, 2011 wakati Man United ya Sir Alex Ferguson ikilambishwa goli 6 kwa 1 pale OT utanielewa ni nini nachomaanisha. Wakati mtukutu Mario Baloteli, Mr ‘Why Always Me’ akitakata kwenye mchezo huo Kun Aguero alikuwa na kazi moja tu ya kuwapindua pindua wakina Rio Ferdinand, Chris Smalling, Patrice Evra na Jonny Evans na kama hawakulala na viatu siku ile basi walilala kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, what a striker.

Michezo 384, magoli 257 ndani ya uzi wa bluu bahari wa watoto wa Etihad, huyu ndiye mwanaume aliyemaliza ukame wa miaka 44 ya City kutotwaa EPL na kupeleka kilio kwa majirani Manchester United ambao tayari kombe walikuwa wamekwishalishikilia mkono mmoja, kwa goli lake la dakika ya 90+5 msimu wa mwaka 2011/12 kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya QPR, Full Time Man City 3 vs QPR 2 huku Man United ambao walikuwa wametulia pale Stadium of Light mechi yao ilikuwa imekwishamalizika dakika 2 mbele na tayari walikuwa wamemtwanga Sundeland 1 – 0 na sasa walikuwa wanasubiri matokeo ya City apate sare tu au apoteze ili wakabidhiwe kombe lao.

Hadi dakika ya 90, City alikuwa kashapigwa 2 kwa 1 na QPR lakini baada ya dakika 5 za nyongeza ndipo maajabu yalipotokea kwa City kuchomoa na kuongeza msumari wa 3 uliochomekwa na Muargentina, Sergio Kun Aguero, ligi inamalizika City na United wote wameshinda michezo 28, wote wamesare michezo 5 na kupoteza michezo 5 wakiwa na alama sawa 89, City wanachukua ndoo ya EPL msimu wa 2011/12 baada ya kipindi kirefu kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa.

Wiki hii zimetoka taarifa za Sergio Kun Aguero kuachana rasmi na klabu ya Manchester City mwishoni mwa msimu huu mara baada ya miaka 10 akiwa ametwaa mataji 10, tutammiss sana mwanaume aliyecheka na nyavu wakati wowote alioutaka, mwanaume aliyebadilisha matokeo na kuwafanya City kuwa tishio wakati wote awapo uwanjani, nadhani ukifanya tafiti fupi ya washambuliaji bora kuwahi kutokea kwenye ligi kuu ya nchini uingereza huwezi acha kumtaja Muargentina huyu Sergio Kun Aguero, hatuwezi kumaliza kuzungumzia maajabu yake makubwa aliyowahi fanya uwanjani nadhani tusubiri tuone ni timu gani atakayojiunga nayo mwishoni mwa msimu halafu tutaendelea kumzungumzia zaidi kuanzia hapo.

Wakati Kun Aguero akinipa mshtuko na kuniacha na simamzi ya kutoona tena miguu yake pale Etihad ikifanya kazi ngumu ya kuuchezea mpira kuwa nyepesi kwa upande wa Tanzania pia nimeachwa mdomo wazi huku nisiamini kile ninachokiona, wakati Tanzania ikihangaika kusimamisha uchumi wake na wa wananchi wake ambapo kwa kipindi kirefu ulionekana kulegalega wakati nchi majirani zake zikipiga hatua kubwa za kimaendeleo.

Tanzania iliyopewa a.k.a ya shamba la bibi, chaka la wana, masikini wa kutupwa na nyingine nyingi mwaka 2015 ilikata shauri na kuamua kuingiza serikalini viongozi na watendaji wenye ueledi chini ya Hayati John Pombe Magufuli ili kusimama imara kwenye kuimarisha uchumi wake, kusimamia kidete rasilimali zake na kuziba mianya ya rushwa, wizi, ufisadi na janja ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo ilikuwa ikileta mtikisiko wa kiuchumi na kukwama kwa maendeleo.

Miongoni mwa viongozi walioingia kwenye kipindi hicho ambacho kimekuwa cha mabadiliko makubwa ni mzaliwa wa Kasumo Kigoma Dkt.Philip Mpango ambaye alikuwa ni waziri wa fedha na mipango, tunaweza kusema huyu ndiye alikuwa kiungo mchezeshaji kwenye mambo yote haya ya kimaendeleo tuliyokuwa tukiyaona kwa takribani miaka 6 sasa.

Baada ya mambo yote hayo aliyoyafanya akiwa serikalini, Machi 30, 2021 Jina la Dkt.Philip Mpango liliwasilishwa bungeni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kama mteuliwa wa nafasi ya Makamu wa Rais ambapo akathibitishwa na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa kura za pamoja 363 sawa na 100%. Wengi wameoneshwa kuwa na imani kubwa na uteuzi wa Dkt.Mpango hasa kutokana na taaluma yake na kipindi tunachopitia kwa sasa kama nchi, tunasubiri tuone namna atakavyosimamia mambo mbalimbali na utendaji wake kwenye kufanya kazi na Mhe.rais kwani kwa sasa ndiye atakuwa mshauri wake wa karibu.

Wengi wameonesha wazi kushtukizwa na uteuzi huu kwani hawakuutarajia kama mimi ambavyo sikutarajia kuona Sergio Aguero akiondoka City kipindi hiki, anatoka mtoto wa Argentina mwenye uwezo mkubwa wa kusakata kabumbu kwenye ligi maarufu duniani, anaingia mtoto wa kimaskini kutoka Kigoma kwenye nafasi ya umakamu wa rais ndani ya nchi inayotaka kupiga hatua, nini kitakachotokea?, tusubiri tuone, alimaliza Mzee Gogoki Kigo na kunifanya nishushe pumzi nzito ya kupokea stori hii iliyonipa utulivu kwa muda mrefu.

Ilinibidi nimuombe Mzee Gogoki anikaribishe ndani kwake niweze kutazama vipindi vya Mtazamo ya Masoud Kipanya & Rahma Mwita na Sports Bomba ya Ester Maongezi, Wilson Oruma & Gwamaka Francis kupitia Plus TV channel namba 294 on DStv ili niweze kutazama vizuri taarifa za watu hawa wawili, Dkt. Philip Mpango na Sergio Kun Aguero nami nijue nini cha kusema kuanzia hapo.