Nazivunja Amri za Chama cha Wanaume Afrika Mashariki na Kati (CHAWAMAKA) ibara ya 2 kipengele kidogo cha 10 (a) cha katiba kinachosema, mwanamke apigiwi saluti (Natania😉).

Nasimama kwa ukakamavu na kwa heshima ya kipekee huku mkono wangu wa kushoto nikiukunja vyema nyuma ya kiuno kusudi nisipoteze attention ya nachoenda kufanya sasa kwa maana hili ni kubwa katika hiatoria ya nchi yetu, Afrika na dunia. Ni saluti na nusu kwenda kwa rais wa sita wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na rais wa kwanza mwanamke nchini tangu tumepata uhuru miaka ile ya 1961.

Narudisha kumbukumbu zangu kwa kasi kama ambavyo na wewe unatakiwa kufanya muda huu, unakumbuka wakati ule ukiwa unaumwa?, unakumbuka wakati ule ukiwa una njaa?, ukiwa umeumia au ukiwa na majonzi na jinsi ambavyo Mama alikuwa anasimama na wewe bila kujali upo kwenye hali gani. Ataumia moyoni, atahisi njaa tumboni, atajawa na wasiwasi kichwani, atajipunja/atajinyima kabisa usingizi ili kuhakikisha wewe unakuwa katika hali nzuri na inayofaa.

Simama na umpigie Mama makofi 21 popote pale alipo kwa kuwa hatuna kibali cha kucharaza mizinga 21 kama iliyosikika leo pale Ikulu Magogoni jijini Dar es Salaam wakati Champion mpya aliyewainua wakina Mama, Samia Suluhu Hassan akiapiashwa kama kiongozi mpya wa nchi.

Naamini tupo kwenye mikono salama, kama ilivyo kawaida ukiwa chini ya Mama.

Huenda Machi 17, 2021 ilikuwa ni siku ngumu kwa watanzania tofauti tofauti, wapo waliopoteza fahamu, wapo waliolia, wapo walioumia na pia wapo waliochanganyikiwa pindi tu waliposikia sauti ya aliyekuwa Makamu wa Rais (kwa sasa Rais) Mama Samia Suluhu Hassan akitangaza taarifa za kuondokewa na rais wa awamu ya tano, hayati Dkt.John Pombe Magufuli aliyefariki kwa matatizo ya moyo.

Unafikiri Mama Samia alikuwa haumii wakati wa kutoa taarifa ile ngumu na nzito? Hapana, kama ilivyo kawaida ya wakina Mama wamekuwa wakisimama imara na kuvaa ujasiri mara zote zitokeapo changamoto na kuhakikisha watoto (watu walio chini yake) wananyanyuka tena, wanapata matumaini na kusikia faraja tena.

Huenda tulitegemea taarifa ile ingetolewa huku uso wa Mama Samia ukibubujikwa na machozi na sauti yake ikikwama kwa kwikwi na kilio lakini lahasha aliyaweka maumivu ndani na kuhakikisha watanzania wote wanaipata taarifa ile bila kuvunjwa zaidi moyo, na huyo ndiye Mama.

Kwenye hotuba yake fupi leo mara baada ya kula kiapo cha kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bado alionyesha ukomavu na uwezo mkubwa wa kuwa kiongozi licha ya kuapishwa kwenye kipindi kigumu sana.

Ushindi upo mwanamke nyanyuka.

Mama Samia Suluhu Hassan ameonesha wazi namna ambavyo karama ya uongozi na ujasiri ambao wanao wakina Mama toka mwanzo unavyoweza kufanya kazi hata kwenye nafasi kubwa na ambazo wao huwa wanaamini haziwezekaniki.

Hapo hapo ulipo, Mama Mjasiriamali, Mama Mwalimu, Mama Daktari, Mama wa nyumbani, Mama mfanyabiashara simama imara kwa miguu yote miwili uweze kuyafanya majukumu yako kwa usahihi kwani ishadhihirika wazi kuwa kwa sasa hakuna kinachoshindikana.

Wanawake wanaweza tuendelee kuwapa nafasi

Naangalia namna ambavyo Maimuna Kichogoli mtoto wa Mzee Kichogoli Kamundo aliyekosa haki ya kupata elimu kwa muda mrefu sasa, Baba yake mzazi akiamini kumuozesha ndiyo ushindi sahihi na ndiyo njia salama ya kumpeleka binti yake.

Kwa hili lililotokea, machozi ya Maimuna yatafutwa kwa unifomu safi zitakazoshoneshwa kwa fundi Maiko na Mzee Kichogoli mwenyewe ili Jumatatu binti yake akaanze kuutafuta ushindi wa kuwatoa mavumbini kwa pasi safi ya kisigino kutoka kwenye elimu.

Nasubiri kuona hasira za mabinti wote kwenye kuitafuta mali ambayo mshairi alishasema awali kuwa kama wanaitaka mali basi wataipata shuleni. Mapenzi, starehe na ulevi vinawekwa mkono wa kushoto sasa panatafutwa paleee kwani Mama Samia kashatoboa kama mshale.

Kila kitu kinatokea kwa sababu hakuna cha bahati mbaya.

Ahsante Mwenyezi Mungu kwa kutuletea Dkt.John Pombe Magufuli ambaye ndiye aliyemuamini Mama Samia Suluhu Hassan na kumpa nafasi ambayo kwa kipindi chote aliisimamia vyema.

Tunamshukuru na tutaendelea kumuombea kutokana na utendaji wake uliotukuka kwa kujitoa kwa watanzania na kubwa zaidi ni kutuacha kwenye mikono salama ya Mama ambapo tunaamini kwenye uongozi wake tutavuka kuelekea nchi ya ahadi.

Hongera Mama Samia Suluhu Hassan na ahsante kwa kurudisha matumaini na kuonyesha tena njia ya ushindi kwa wanawake nchini.

Wanaume mpoooo? sasa mkae kwa kutulia!😀