“Kilichotukuta wala hatuwezi kuongea, kweli kifo ni katili umemchukua mpaka tuliyemtegemea!!”

Taarifa zinazosikika kwenye radio kuu kuu ya Bibi Nyasasi Masike kule Bunda Mara asubuhi ya Machi 18, 2021 wakati akivunja vunja baadhi ya vishina vilivyojaa kwenye kiwanja chake alichokipata miaka 3 iliyopita kutoka kwa wenye nguvu ya kipato ambao walimnyang’anya kutokana na nafasi zao ni kuwa mtetezi aliyemshindia vita na kupata haki yake, leo hii hatuko nae tena.

Nasimama kwa kishindo kwenye Daraja la kwanza la juu nchini ‘Flyover’ la Mfugale jijini Dar es Salaam nikiangalia nyuso za huzuni za wamachinga, Mama ntilie na wafanyabiashara wadogo wadogo wote nchini kutokana na kumpoteza rafiki/mpambanaji wao aliyewapigania mara zote bila kuchoka, Jemedari aliyerudisha tumaini kwa watanzania wenye kipato cha chini, Jemedari aliyeusimamia ukweli, Jemedari aliyerudisha afya kwenye maendeleo, utendaji na sekta mbalimbali.

Nayatazama machozi ya furaha ya konda wa daladala ya Gongo la Mboto kwenda katikati ya mji akijisikia fahari kupita kwenye daraja hili la juu ambalo ujenzi wake uligharimu zaidi ya bilioni 106.9 ambapo ndani yake kuna kodi aliyoichangia yeye na watanzania wengine wazalendo. Ni bilioni 106 hizi hizi ambazo awali tulikuwa tukiona zikiwanufaisha na kuwafaidisha wachache waliotutunishia vifua na kuchukua sauti zetu kila tulipotaka kufungua kinywa kuzungumza juu ya ulafi wao lakini kwenye kipindi kifupi Mzee aliturudishia sauti zetu na mambo yakawa mswano.

“Hata kama ni mzazi
Saa zingine nawaza nikuchukie
Sema tu we ni mzazi
Acha ukweli wako nikwambie

Daddy iii, naongea na wewe eh
Daddy iii, naongea na wewe
Naongea na wewe”

Kamlio ka wimbo wangu pendwa ambao pia ulikuwa ni wimbo pendwa wa Jemedari kanalia kwenye simu yangu ishara ya kwamba kuna siku inaingia/inapigwa, ndiyo ni wimbo pendwa wa Jemedari kutoka kwa Stamina aliomshirikisha Prof.Jay & One Six – Baba, Jemedari mara zote alionyesha mapenzi yake ya wazi kwenye sanaa na michezo kwa ujumla nchini, unakumbuka simu yake kwenda kwa Mwana Fa wakati hana hata ndoto za kuwa atakuja kuwa Mbunge?, simu ya kwenda kwa Alikiba je, ukiacha ile ya Diamond Platnumz pale Kigoma anyways tuachane na hayo, unakumbuka ile furaha yake mara baada ya timu yetu ya Taifa kufuzu kwenye michuano ya Afcon baada kipindi kirefu?

Tusihuzunike sana Jemedari ajatuacha pabaya, alishairasimisha sanaa kama sekta rasmi, Indoor Arena itakayowawezesha wasanii kufanya matamasha yao na kukusanya watu wengi ipo kwenye mchakato wa kujengwa lakini hata ramani ya ule uwanja mkubwa wa michezo jijini Dodoma tumekwishaiona.

Acha nipokee simu yangu nijue ni nini kinachojiri maana inaita kwa muda mrefu bila kukata, anhaa ni simu kutoka Dawasco ikinipa majibu kuhusu changamoto ya maji kuvuja nyumbani kwangu niliyoiripoti dakika kadhaa zilizopita.

Tunashukuru changamoto ya maji kwa sasa imepatiwa suluhisho kwenye maeneo mengi tofauti na awali kama ilivyo kwenye umeme ambao umekuwa wa bei nafuu ambao kila mtanzania anaweza kumudu gharama zake na ni wa uhakika.

“Sitafsiriwi kwa haya, machozi na magumu
Mimi ni mshindi tu, kamusi ndiye Mungu”

Kalamu inagoma kuandika, kutokana na yake mengi mazuri yasiyo na idadi, Ahsante kwa kututoa matopeni/usingizi, ahsante kwa kutuinua kwenye kila sekta, ahsante kwa kuwaamini vijana, ahsante kwa kurudisha heshima na ushindi tena kwa taifa.

Jino la dhahabu, jino kali, Jino imara  lililorudisha utimamu wa kuvunja vunja kila kiingiacho kinywani mwetu kabla ya kuingia tumboni (nchini)

Madini tuliyathabiti tukaanza kuona faida zake, uchumi ulikuwa, maendeleo yalikuwa ya wazi wazi, tusiyoyategemea yamewezekana, Magufuli Baba Lao.

Umevipiga vita vilivyo vizuri hakika mwendo umeumaliza, Ahsante JPM, Pumzika kwa Amani rafiki wa wanyonge usiyejivika makuu, Pumzika kwa Amani Dkt.wa Kufichua uovu, Dkt.kutibu ufisadi na ubadhilifu wa mali za umma, Dkt.wa kutibu uzembe na uonevu.

Sisi ni matajiri, tutaendelea kuchapa kazi ili tule, tutakuwa na hofu kubwa ya Mungu katika kila kitu na mara zote tutausimamia ukweli, Ahsante kwa matibabu ya kifikra uliyotuachia Daktari John Pombe Joseph Magufuli.

Pumzika kwa Amani Mjamaa wa Wanyonge, Pumzika kwa Amani Mpenda haki, Pumzika kwa amani rafiki wa konda wa Gongo la Mboto, Pumzika kwa Amani Rais John Pombe Joseph Magufuli.