Tuzo za 63 za Grammy kwa mwaka huu wa 2021 zimefanikiwa kufanyika usiku wa Machi 14, 2021 kwenye ukumbi wa Los Angeles Convention Center uliopo Los Angeles nchini Marekani ambapo ilishuhudiwa nguli wa muziki wa Pop duniani, Beyonce na wakali wa Nigeria Burna Boy na Wizkid wakiandika historia kwenye usiku wa tuzo hizo.

Beyonce ambaye alikuwa akiingia kwenye tuzo hizo kama mwanamke pekee anayeshikilia rekodi ya kutajwa mara nyingi zaidi kwenye vipengele vya kuwania tuzo za Grammy akiwa ametajwa mara 79 mpaka sasa, amefanikiwa kuweka rekodi mpya ya kuwa mwanamke wa kwanza kushinda tuzo nyingi zaidi za Grammy, tuzo 28 baada ya kuondoka na tuzo nne kati ya tisa usiku wa Machi 14, kwenye vipengele vya Best R&B performance kupitia wimbo wa Black Parade, Best rap song kupitia wimbo wa Savage alioshirikishwa na Megan Thee Stallion ambao pia ulishinda kwenye kipengele cha Best rap performance na Best music film ambapo alishinda kupitia wimbo wa Black Is King.

Wakati huo huo nyota ya wasanii wa Afrika imeendelea kung’aa kwenye anga la kimataifa mara baada ya wakali wawili kutoka nchini Nigeria, Burna Boy na Wizkid kufanikiwa kutwaa tuzo usiku huo. Burna Boy amefanikiwa kutwaa tuzo kupitia Album yake ya Twice as Tall kwenye kipengele cha Best global music album huku Wizkid akishinda tuzo kupitia wimbo wa Brown Skin Girl alioshirikishwa na Beyonce kwenye kipengele cha Best Music Video.

Washindi wengine ni Record of the year iliyokwenda kwa Billie Eilish kupitia wimbo wa Everything I Wanted, Album of the year iliyokwenda kwa Taylor Swif kupitia Album ya Folklore, Song of the year ikienda kwa H.E.R kupitia wimbo wa I Can’t Breathe, huku Best pop solo performance ikienda kwa Harry Styles kupitia wimbo waWatermelon Sugar.