Mstahiki Meya mpya wa Jiji la Dar es Salaam, Omari Kumbilamoto amesema kuwa Jengo la Machinga complex ni miongoni wa urithi wenye changamoto waliourithi kutoka kwenye jiji la zamani la Dar es salaam. Mhe.Kumbilamoto ameyasema hayo Jumatatu ya Machi 15,2021 kwenye kipindi cha Sebuleni cha Plus TV na Gift Swai, Sikawa Junior na Kevin Lameck kinachoruka mubashara kupitia kinga’amuzi cha DStv channel namba 294.

“Jengo la Machinga Complex siyo rafiki kwa wafanyabiashara, lile ni moja la mabalaa ya asili tuliyorithi sisi Jiji la Dar es Salaam kwani bado kuna deni kubwa” – Mstahiki Meya wa Jiji la DSM, Omari Kumbilamoto

Aidha,Kumbilamoto amesema moja ya makosa makubwa yaliyofanywa kwenye ujenzi wa jengo hilo uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 12.7 za kitanzania ni kwa viongozi kutowashirikisha wafanyabishara ambao ndiyo watumiaji wakubwa wa jengo hilo kabla ya kuchukua hatua za kuanza ujenzi.

Ikumbukwe Jengo la Machinga Complex lililopo eneo la Karume jijini Dar es salaam limekuwa kwenye sintofahamu ya muda mrefu hasa kutokana na kuwepo kwa mkanganyiko kwenye gharama zilizotumika kwenye ujenzi wake ambazo ni shilingi bilioni 12.7 za mkopo kutoka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na sasa gharama za urudishaji mkopo huo ambapo hadi mwaka 2017 zilifikia shilingi bilioni 40.