Bondia Hassan Mwakinyo ambaye anatarajiwa kushuka ulingoni Machi 26 mwaka huu pale Next Door Arena kuzichapa dhidi ya Mzimbwabe Brendon Denes wakiwania mkanda wa ABU kwenye usiku wa mapambano ya Rumble In Dar unaodhaminiwa na Benki ya KCB na kurushwa mubashara kupitia Plus Televison channel namba 294 kwenye king’amuzi cha DStv, amekanusha vikali taarifa za kutumia ushirikina pamoja na kuchagua mabondia wa kuingia nao ulingoni ili kuepuka kushindwa kwenye mapambano yake.

Mwakinyo ameyasema hayo kwenye mahojiano ya kipindi cha Sebuleni cha Plus TV na Gift Swai, Sikawa Junior & Kevin Lameck Ijumaa ya Machi 12, 2021, Mwakinyo amesema yeye huwa yupo tayari kupambana na bondia yeyote endapo tu makubaliano na maandalizi ya promota yakiwa sawa sawa na kusisitiza kuwa yeye ni mtu mwenye hofu ya Mungu na huwa anamuomba Mungu kabla ya kwenda kwenye pambano lake  lolote lile na ndiye sababu kubwa ya yeye kuibuka na ushindi tofauti na wanaosema kuwa anatumia nguvu za giza ambazo ndizo zinazomuwezesha kushinda mapambano yake.

“Mimi naamini kitu kinachotubeba sisi ni mazoezi na tuna imani na dini zetu na tunaombewa na watu wetu hicho ndicho kinachotubeba na si ushirikina”

“Kama kungekuwa na nafasi ya ushirikina kwenye boxing basi watoto wa waganga wote wangekuwa mabingwa wa dunia, Nigeria mpaka leo wangekuwa wameshika michezo yote mikubwa duniani” – amesema Mwakinyo

Aidha Bondia huyo ameonyesha kuchukizwa wazi na baadhi ya viongozi wa mchezo wa ngumi nchini ambao wanayaficha matatizo ya mchezo huo na kutanguliza maslahi yao binafsi hivyo kupelekea mazingira magumu na hali mbaya kwa mabondia na watu mbalimbali wanaohusika na mchezo huo huku akikumbushia tukio la mmoja wa viongozi wa ngumi nchini kuzungumzia chakula badala ya matatizo ya mchezo huo walipopata nafasi ya kupata chakula cha mchana na rais.

 

“Tuliwahi kupata mualiko wa kwenda kula chakula cha mchana na Mhe.Rais na baadae akataka kujua changamoto za mchezo wa boxing lakini mmoja wa viongozi alipopewa nafasi ya kuzungumza yeye akausifia msosi badala ya kueleza matatizo” –  Hassan Mwakinyo

Usiku wa mapambano ya Rumble In Dar ulioandaliwa na Jackson Group kwa kushirikina na Onomo Hotel, Plus TV, DStv Tanzania, KCB Bank na bodi ya utalii unategemewa kuhodhi mapambano zaidi ya nane ambayo yote yatakuwa mubashara kupitia DStv channel 294, Plus TV.