Zilikuwa ni takribani dakika 210 za kwenye viwanja vya Estádio do Dragão na Juventus Stadium zilizofuta ndoto za wababe wa Italy, Juventus na nyota wake Cristiano Ronaldo kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya ikiwa ni muendelezo wa matokeo ya kusuasua ya klabu hiyo msimu huu kwenye michuano mbalimbali chini ya kocha wake Andrea Pirlo.

Hii inakuwa ni mara ya kwanza baada ya miaka 16 kwa mshambuliaji wa timu hiyo raia wa Ureno, CR7 kushindwa kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya ligi ya Mabingwa barani Ulaya akiwa na vilabu vya Manchester United, Real Madrid na sasa Juventus ambapo mara ya mwisho kushindwa kufuzu hatua ya robo fainali ilikuwa ni mwaka 2005 ambapo Man United iliondolewa na Mabingwa wa Italy kipindi hicho, Ac Milan kwenye hatua ya 16 bora.

Kama ilivyotokea kwa Cristiano, vivyo hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa hasimu wake mkubwa Lionel Messi, ambaye naye usiku wa Machi 10, 2021 ameshindwa kufuzu hatua ya robo fainali ya ligi ya Mabingwa barani Ulaya kwa mara ya kwanza baada miaka 16 kutokana ya timu yake ya FC Barcelona kufurumushwa kwa jumla ya mabao 5 kwa 2 na Paris Saint Germain ya Kylian Mbappe kwenye hatua ya 16 bora.

Unahisi hizi ni zama za mwisho za nyota hawa wawili Cristiano Ronaldo na Lionel Messi kuendelea kutikisa kwenye ramani ya soka duniani?

Ungana na Ester Maongezi, Gwamaka Francis na Wilson Oruma kwenye Sports Bomba ya Plus TV kuanzia saa 2:30 za usiku kupitia king’amuzi cha DStv channel 294, kujua hatma ya miamba hawa.