Kuelekea mpambano mkubwa wa Rumble In Dar Second Edition, usiku wa Machi 26, 2021 ambapo mabondia wa kitanzania Hassan Mwakinyo, Shaaban Jongo na Ibrahim Class watashuka ulingoni kupambana na mabondia wengine kutoka nje ya nchi pale Next Door Arena, leo Machi 11, 2020 waandaaji na wadhamini wa mapambano hayo walikuwa wakizungumza na wanahabari kwenye Hoteli ya Onomo, iliyopo Posta jijini Dar es salaam.

Mapambano hayo ambayo yatakuwa LIVE kwenye zaidi ya nchi 32 barani Afrika kupitia Plus Television katika kisimbuzi cha DStv channel namba 294, yatawakutanisha mabondia kutoka nchi tofauti tofauti duniani na pia yatakuwa mubashara barani Ulaya, Asia na Amerika kupitia OTT Platform ya Fite TV.

Mkurugenzi Mkuu Jackson Group, Bw.Kelvin Twissa ambao ndiyo waandaaji wakuu wa mapambano hayo amesema kuwa ngumi hizo zitakuwa na mvuto wa kipekee kutokana na ubora wa mabondia watakaoshuka ulingoni siku hiyo huku Bi.Christina Manyenye, Mkuu wa Masoko KCB Bank ambao ndiyo wadhamini wakuu wa mapambano hayo amesema wao kama KCB wanaendelea kuonesha nia yao ya dhati ya kuinua sekta ya michezo nchini kwa kuendelea kujikita kwenye kudhamini michezo tofauti tofauti.Aidha, Mkurugenzi wa uendeshaji wa Plus TV, Mr Ramadhan Bukini na Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Multichoice Tanzania Mr.Baraka shelukindo ambao wao ndiyo washirika wakuu wa kurusha ngumi hizo kupitia Plus TV kwenye king’amuzi cha DStv wamesema, Plus TV inaendeleza maono yake ya kuhakikisha vipaji vya vijana wengi wa kitanzania vinaonekana kwenye mataifa mengi zaidi tena kwenye ubora mkubwa.Bondia Hassan Mwakinyo ambaye atakuwa ni miongoni mwa mabondia watakaoshuka ulingoni siku hiyo, amesema yeye yupo tayari kwa mpambano wake huku akiahidi ushindi kwa watanzania,

“Ahadi yangu kwenye pambano hili ni kuonyesha kiwango cha Boxing kwa hiyo haraka yake ndiyo itakayomfanya amalize pambano, anatakiwa ajue anacheza na boxer hatari”

“Naahidi kuwa nitafanya vizuri kwenye mchezo wa Machi 26 na moja ya vitu ambavyo vinamuonesha Bondia kuwa fiti ni kufanya vile alivyoahidi katika ulingo” – alisema Mwakinyo

Kwa upande wa Ibrahim Class naye amejigamba kuibuka kidedea kwenye mchezo wake kwa kumdondosha mpinzani wake mapema,

“Mimi nimejiandaa vizuri katika mpambano unaokuja, napenda niwaaminishe watanzania kuwa hata pambano lingekuwa leo au kesho nipo tayari kupigana”

“Huwa nabadilika badilika kama kinyonga sina mtindo mmoja wa kupigana, utakavyokuja ndivyo utakavyopigwa” – Ibrahim Class

Popote ulipo Afrika unaweza kushuhudia mapambano haya ya Rumble In Dar usiku wa Machi 26, LIVE on DStv channel namba 294 kwa kulipia sasa kifurushi chako cha DStv Bomba kwa gharama ya shilingi 19,900/= tu.