“Huenda kelele za mashabiki wa klabu ya Man United zimeanza kuzaa matunda”.

Klabu ya Manchester United leo Machi 10, 2021 imewatangaza John Murtough kuwa Mkurugenzi wake wa kwanza wa masuala ya soka na kiungo wa zamani wa klabu hiyo raia wa Scotland, Darren Fletcher kuwa Mkurugenzi wa kwanza wa benchi la ufundi.

Hatua hii inakuja mara baada ya kelele na malalamiko ya takribani miaka sita ya mashabiki wa klabu hiyo kuhitaji wakurugenzi wa benchi la ufundi kutokana na sintofahamu zilizokuwa zikijitokeza kwenye masuala ya usajili ya ndani ya timu hiyo ambapo Mtendaji Mkuu wa klabu, Ed Woodward ndiye aliyekuwa akishughulika na masuala ya usajili.

Ed Woodward

John Murtough ambaye kwa sasa atakuwa akihusika kwa kiasi kikubwa na masuala ya soka ya United, tayari alikuwa katika ajira ndani ya klabu hiyo, kama Mkuu wa maendeleo ya mpira wa miguu na amekuwa klabuni hapo tangu mwaka 2013 ambapo awali alikuwa akifanya kazi na kocha wa sasa wa West Ham United, David Moyes kwenye klabu ya Everton.

Murtough pia alikuwa ni miongoni mwa sehemu ya watu muhimu katika akademi ambayo iliwakuza na kuwatengeneza nyota raia wa Uingereza Wayne Rooney na Ross Barkley.

Kwa upande wa Darren Fletcher ambaye yeye aliitumikia Man United kwa mafanikio makubwa kwa zaidi ya miaka 10, mapema mwaka huu aliteuliwa kuwa ni mmoja wa walimu kwenye benchi la ufundi la kikosi cha kwanza cha Manchester United chini ya kocha mkuu Ole Gunnar Solskjaer akitokea kikosi cha chini ya umri wa miaka 16.

Kwa taarifa zaidi za kimichezo za nje na ndani ya nchi, ungana na Gwamaka Francis, Esther Moangezi na Wilson Oruma kupitia kipindi cha Sports Bomba cha Plus TV kila siku za Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa 2:30 za usiku kupitia kisimbuzi cha DStv channel namba 294.