Ni majira ya saa 1 na dakika 47 za usiku taratibu nikiwa kwenye usafiri wa daladala kurejea nyumbani mara baada ya mihangaiko ya hapa na pale ya kutwa nzima. Kelele za wapiga debe zilikuwa zikivuma kwa kasi na kuyapa masikio yangu taarifa ya kila kituo ambapo daladala niliyokuwamo ilikuwa ikisimama kushusha na kubeba abiria wengine waliokuwa wakielekea maeneo ya Sinza, jijini Dar es Salaam.

Ilikuwa ikituchukua takribani dakika 2 na sekunde kadhaa kwenye zoezi la daladala yetu kusimama kushusha abiria lakini pia kuwabeba abiria wengine kwenye kila kituo lakini hali ilikuwa tofauti kidogo kwenye moja ya kituo cha daladala ambapo tofauti na mazoea ya muda mfupi tuliyojijengea ya gari kutosimama zaidi ya dakika 2 kituoni, hapa ilituchukua zaidi ya dakika 6 kutokana na mzozo uliokuwa ukiendelea kati ya mpiga debe na kondakta wa gari yetu ambapo kwa

pamoja walionekana kutokuelewana kwenye suala zima la malipo mara baada ya mpiga debe kufanya kazi ya kuitia abiria kwenye gari lile.

Hali halisi ilikuwa hivi, mara baada ya mpiga debe kuita abiria, kondakta akatoa shilingi 500 na kumpatia mpiga debe ili achukue shilingi 300 kama ujira wa kazi aliyoifanya muda huo na shilingi 200 inayobaki amrudishie kondakta lakini mpiga debe alikataa kurudisha hiyo shilingi 200 kwa madai ya kuwa alishawahi kuita abiria kwenye gari hiyo hiyo siku kadhaa zilizopita lakini hakupatiwa ujira wake na badala yake Kondakta alimkimbia hivyo leo kuchukua shilingi 500 yote ni kulipia pia deni lake la nyuma au kulipa kisasi kutokana na ujanja aliofanyiwa siku ile.

Jambo hili lilinikumbusha mipango na makonde ya kiufundi yaliyokuwa yakirushwa

na bondia Anthony Joshua ulingoni kwenye mchezo wake wa marudiano dhidi ya kibonge mwepesi, Andy Ruiz Jr pale Diriyah Arena, Diriyah, Saudi Arabia usiku wa Desemba 7, 2019 mara baada ya kufanya makosa na kuchezea kichapo cha aibu kwenye pambano la awali pale New York’s Madison Square Garden kwenye raundi ya saba tu ya mchezo, usiku wa Juni 1, 2019.

Huenda kila mtu huwa anahitaji nafasi nyingine ili kuweka msawazo, kulipa deni au kulipa kisasi mara baada ya kukosea kwenye kufanya jambo fulani kwa mara ya kwanza. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa mpiga debe ambaye mara ya kwanza alizubaa akapigwa chenga na kondakta lakini mara ya pili akasimama imara, akasuka mipango mizuri na akafanikiwa kulipa kisasi, vivyo hivyo kwa Anthony Joshua ambaye nae alisimama imara na kufuta makosa aliyoyafanya kwenye mchezo wake kwa kwanza na akafanikiwa

kulipa deni dhidi ya Andy Ruiz Jr.

Jambo kama hili lipo pia kwenye mchezo wa Boxing nchini, wapo mabondia waliofanya makosa mara ya kwanza na kupelekea kupoteza mapambano na mikanda yao waliyokuwa wakiishikilia hivyo kwa sasa wanahitaji nafasi nyingine ili waweze kuweka msawazo kwenye hilo.

Plus Television kwa kushirikiana na DStv Tanzania wameliona hilo na ndiyo maana wamekuja na usiku wa kulipa madeni, usiku wa kuweka msawazo, usiku wa kumaliza ubishi, Usiku Wa Kisasi utakaofanyika viwanja wa Kinesi, Jijini Dar es Salaam, Februari 27, 2021 kwa kushuhudiwa mapambano ya kukata na ngebe zaidi 8 na pambano kuu 1.

Ni bondia Francis Miyeyusho dhidi ya Habibu Pengo huku Haidari Mchanjo akiumana na Muksini Swalehe, Mfaume Mfaume dhidi ya

Yusufu Mbembe, Baina Mazola dhidi ya Ismail Galiatano, Bakari Magona dhidi ya Emmanuel Mwakyembe, Luckman Ngambongali atazichapa na Mohamed Mpombo, huku Waziri Mbonde akiumana na Mwinyi Mzengela, George Bonabucha dhidi ya Hashimu Zuberi na Ibrahim Makubi dhidi ya Iddi Mbaraka.

Mapambano yote haya yataruka mubashara kupitia Plus Television channel namba 294 kwenye king’amuzi cha DStv, Februari 27 kuanzia saa 3 kamili za usiku, lipia sasa kifurushi chako cha DStv Bomba kwa gharama ya shilingi.19,990 tu, uweze kujua nani ni nani kwenye Usiku wa Kisasi LIVE on Plus TV.