Klabu ya Simba Sports Club imemsimamisha kiungo wake wa kati na nahodha wa zamani wa timu hiyo, Jonas Mkude ambaye ndiye mchezaji mkongwe zaidi kwa sasa kwenye kikosi hicho kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu.

Klabu ya Simba imetoa taarifa hiyo kupitia mitandao yake ya kijamii ikiwa ni siku kadhaa tu tangu watoke kupata ushindi mnono wa magoli 5 kwa bila kwenye mchezo wa FA dhidi ya Majimaji FC ya Songea.

Kwenye taarifa yao, Simba wamesema kuwa wamemsimamisha mchezaji huyo kwa sasa ili kupisha uchunguzi wa sakata hilo la kinidhamu kwani hadi sasa haijawekwa wazi ni matendo gani au vitu gani vya utovu wa nidhamu alivyovitenda.

Kutokana na rungu hilo, Jonas Mkude sasa huenda akaukosa mchezo wa marudiano wa klabu bingwa barani Afrika kati ya timu yake ya Simba dhidi ya FC Platnum ya Zimbabwe unaotarajiwa kupigwa Januari 6,2021 kwenye uwanja wa B.W.Mkapa Jijini Dar Es Salaam.