Bondia Cosmas Cheka kutoka Dar es Salaam ameendeleza ubabe wake kwenye mchezo wa masumbwi mara baada ya kumtwanga Bondia Mwinyi Mzengela kwa K.O raundi ya 4 usiku wa kuamkia leo, kwenye pambano la Dodoma Boxing lililopigwa kwenye ukumbi Chinangali Park jijini Dodoma.

Pambano hilo la raundi 10 lililorushwa mubashara kupitia Plus TV channel namba 294 kwenye kisimbuzi cha DStv lilitanguliwa na mapambano mengine 7 ya awali na kushuhudiwa likimalizika kwenye raundi ya 4 dakika ya 2 baada ya Cosmas Cheka kumtwanga kwa Knockout (KO), Mwinyi Mzengela.

Hili linakuwa ni pambano la 44 rasmi kwa Bondia Cosmas Cheka huku ukiwa ni ushindi wake wa 25 na 6 kwa K.O

Cheka anaingia kwenye rekodi ya mabondia wachache wa kitanzania waliofanya vizuri ndani ya mwaka 2020 ukiachilia mbali, Bondia Hassan Mwakinyo na Idd Pialari aliyemchapa Mfilipino, Arnel Tinampay miezi kadhaa iliyopita kwenye pambano la raundi 10 pia.