Shirikisho la soka duniani FIFA usiku wa kuamkia leo limetoa tuzo za ‘The Best FIFA Football Awards’ kwa wanasoka na wadau mbalimbali wa mchezo wa mpira wa miguu waliofanya vizuri ndani ya mwaka huu wa 2020.

Tuzo hizo zilizofanyika kwa njia ya mtandao ili kuepuka mkusanyiko ambao ni miongoni mwa vizuizi dhidi ya COVID-19, zilishuhudiwa kwa mara ya kwanza baada ya takribani miaka 10 utawala wa wafalme wawili Mreno, Cristiano Ronaldo na Muargentina, Lionel Messi kwenye tuzo hizo ukivunjwa na raia wa Poland, Robert Lewandowski.

 

Lewandowski anayekipiga kwenye klabu ya Bayern Munich na timu ya taifa ya Poland aliwabwaga mafahali hao wawili baada ya kuchukua tuzo ya Mchezaji bora wa kiume.

Tuzo zingine zilishuhudiwa zikienda kwa;

Kocha Bora wanaume, Jurgen Klopp wa Liverpool.

Kocha bora wanawake, Sarina Wiegman wa Uholanzi.

Mchezaji bora wanawake, Lucy Bronze wa Manchester City.

Golikipa bora wanaume, Manuel Neuer wa Bayern Munich.

Golikipa bora wanawake, Sarah Bouhaddi wa Olympic Lyon.

Goli bora la mwaka, Heung min Son wa Tottenham.

Tuzo ya shabiki bora imeenda kwa Marivaldo Francisco Da Silva wa klabu ya Sports Club do recife ambaye alipata tuzo hiyo kutokana na mapenzi yake ya dhati kwa mchezo wa soka ambapo alilazimika kutembea zaidi ya Kilometa 60 kwa saa 11 kufika uwanja wa Club do recife na mpaka sasa Mbrazil huyo hajawahi kukosa mchezo wowote wa nyumbani wa klabu yake.

Kwa upande wa tuzo ya The FIFA Fair Play Award imeenda kwa Kinda wa miaka 17, Mattia Agnese ambaye yeye aliokoa maisha ya mchezaji wa Cairese, Matteo Briano ambaye alizimia uwanjani kwenye mchezo kati ya Ospedatti dhidi ya Cairese kwa kumpa huduma ya kwanza kumsaidia kupumua.

Na kikosi bora cha mwaka cha wanaume kinaundwa na Manuel Neuer anayesimama kama Mlinda Mlango huku mabeki wakiwa ni Trend Alexander Arnold, Alphonse Davies, Virgil Van Dijk na Sergio Ramos.

Viungo ni Thiago Alcantara, Joshua Kimmich na Kelvin De Bruyne huku washambuliaji wakiwa ni Robert Lewandowski, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.