Kampuni ya Sony Music Entertainment Africa imemteua Christine Mosha, ‘Seven Mosha’, kuongoza na kusimamia Masoko na Maendeleo ya wasanii kwa ukanda wa Afrika Mashariki.

Seven ambaye kwa sasa anamsimamia msanii Ommy Dimpoz kupitia label yake ya Rockstar Africa, atakuwa akiripoti moja kwa moja kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Sony Music Africa, Mr.Sean Watson.

“Seven ametumia sehemu kubwa ya maisha yake kuikuza tasnia ya burudani Afrika, yeye ni mtetezi mwenye chachu ya kukuza kila kitu cha Afrika Mashariki kufika ulimwenguni, ”

“Kwa miaka kadhaa tayari amekuwa mshirika muhimu kwetu, akitoa ufahamu wake wa kipekee na njia bora za kufanya kazi ndani ya Afrika Mashariki .”

“Kwa hivyo tunafurahi kuwa naye kwenye bodi katika kusaidia kukuza orodha yetu ya wasanii wa Afrika Mashariki na kuonyesha ukubwa wetu wa kimataifa kwa wasikilizaji wapya.” alisema Watson

Naye Seven Mosha ameoneshwa kufurahia kupata nafasi hiyo na kuahidi kuendeleza juhudi kubwa anazozifanya kwenye kukuza sanaa ya muziki barani Afrika.

“Nimefurahi sana kujiunga na Sony Music Africa ninatarajia kuendeleza umuhimu katika tasnia nzima ya burudani, sio Afrika Mashariki tu bali katika bara zima”.

Seven ana uzoefu wa zaidi ya miaka 15 kwenye tasnia ya burudani ya Afrika na amefanya kazi kwa karibu na Sony Music Africa kwa miaka mingi

Mwaka 2017 alianzisha kampuni yake ya Rockstar Africa, ambapo alifanikiwa kufanya kazi na wasanii kadhaa wa Afrika Mashariki chini ya kampuni hiyo wakiwemo Lady Jaydee, Ray C, TID, Rose Muhando, Xtatic, Alikiba na Ommy Dimpoz.