Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Ibrahim Mussa almaarufu kama Roma Mkatoliki ametangaza rasmi kuachia kazi yake ya mwisho kwenye career yake ya muziki muda wowote kuanzia sasa.

Roma ambaye amejichimbia nchini Marekani kwa zaidi ya miezi 11 sasa, ametoa taarifa ya kuachia wimbo huo ambao utakuwa wimbo wake wa mwisho kupitia ukurasa wake wa Twitter, Jumanne ya Desemba 8, 2020.

“Wimbo wangu wa kwanza niliutoa mwaka 2007

Wimbo wangu wa mwisho ninautoa muda wowote kuanzia sasa!!Na huu ndiyo utakuwa wimbo wangu wa mwisho!

Asanteni kwa kuwa nami na kuni-support kwa kipindi chote cha miaka 13 niliyowahudumia kwenye sanaa hii ya muziki!”

Bado haijajulikana kama Roma amemaanisha kweli hicho alichokiandika kuwa ataacha muziki baada ya kazi hiyo au ‘wimbo wangu wa mwisho’ ni jina la wimbo huo mpya ama ni baadhi ya mistari iliyopo kwenye ngoma hiyo.

Endapo rapa huyo ataacha kufanya muziki, ataongeza listi ya mastaa wa kitanzania waliotangaza kuacha kufanya muziki ndani ya mwaka 2020, akiwemo C.EO wa Mdee Music, Vanessa Mdee na Mwanadada Jolie.