Plus Television imezindua rasmi msimu wake mpya wa runinga unaofahamika kama
‘Zaidi Na Zaidi’ leo ijumaa ya Novemba 20, 2020 unaokuja na vipindi vipya vitano kuelekea mwishoni mwa mwaka 2020.

Plus TV inayopatikana kwenye zaidi ya nchi 36 barani Afrika kupitia kisimbuzi cha DStv channel namba 294 imeendelea kujikita zaidi kwenye kuzalisha maudhui pendwa na rafiki kwa walaji wake hasa vijana kwa kutambulisha vipindi hivyo vipya ambavyo ni Vamia Jiko kitakachoongozwa na muigizaji mashuhuri na mjasiriamali Esha Buheti, Ina Who? kitakachoongozwa na Salma Kungwi, Being A Star kitakachoongozwa na msanii Lulu Diva, Ndondi Series itakayoruka kwa muda wa miezi mitatu ikiwa ni mjumuisho wa mapambano ya mabondia wa ndani wakishindania mkanda wa UBO na kipindi cha On Air kitakachoongozwa na Izzo Bizness, Jimmy Jamal & Niffer.

Mtangazaji mpya wa On Air, Jimmy Jamal ambaye pia ametambulishwa kama mtangazaji mpya wa Plus TV kwenye hafla hiyo iliyofanyika Oasis Village & Club Mbezi Beach, amewataka wapenzi na mashabiki wote wa sanaa nchini wajiandae kupokea mapinduzi mapya yatakayoenda kuibeba sanaa ya Tanzania kwa kusikia na kuona vitu vipya kupitia On Air ya Plus TV.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa msimu mpya wa ‘Zaidi Na Zaidi’ Mkurugenzi uendeshaji wa Plus TV, Mr. Ramadhani Bukini amesema wao kama Plus TV katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita walijikita zaidi kwenye kuzalisha maudhui bora yanayoenda kwenye uelekeo wa kuwaelimisha na kuwaburudisha watu hasa mambo yanayowahusu moja kwa moja na sasa baada ya mwaka mmoja wanaona ni muda muafaka wa kuongeza yale waliyokuwa wakiyafanya katika kipindi cha mwaka mzima.

Mkuu wa Kitengo cha Masoko kutoka Multichoice Tanzania ambao ni partners wa Plus TV kupitia kisimbuzi chao cha DStv, Baraka Shelukindo amesema wao walipoanza safari na Plus TV walitegemea kuwa mambo yatakuwa mazuri lakini kwa sasa kuona mambo yanakuwa mazuri zaidi ni jambo linalowafurahisha wao kama DStv na watanzania wote.

“Tulipoanza safari hii na Plus TV tulitegemea mambo yatakuwa mazuri lakini kuona leo yanazidi kuwa mazuri ni jambo ambalo linatufurahisha zaidi sisi DStv na watanzania”

“Plus TV kuwepo ndani ya DStv ni fursa kwa watanzania kuonesha vitu na ubora ambao tunao huko kwa wenzetu kwa sababu Plus TV inaonekana kwenye Nchi zaidi ya 36 Afrika” – Mkuu wa kitengo cha masoko MultiChoice Tanzania Baraka Shelukindo

Aidha, Plus TV imewataka watanzania wote kukaa tayari kwa ajili ya kushuhudia pambano la kimataifa na la kihistoria litakaloruka mubashara kupitia Plus TV moja kwa moja kutokea ukumbi wa Next Door Arena Masaki, likiwakutanisha mabondia Idd Pialari kutoka Tanzania na Arnel Tinampay kutoka Ufilipino kwenye pambano la raundi 10 litakalotanguliwa na mapambano mengine saba ya utangulizi ya mabondia wa ndani.

Pambano hilo linalotarajiwa kupigwa usiku wa Novemba 28, kuanzia majira ya saa 3 za usiku litaonekana moja kwa moja kupitia Plus TV pekee kwenye kisimbuzi cha DStv ndani ya kifurushi cha Bomba kwa gharama ya shilingi 19,900 tu.