Mbunge wa Kongwa na aliyekuwa Spika wa Bunge la 11 la Jamhuri la Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amefanikiwa kurejea tena kwenye nafasi hiyo mara baada ya kuchaguliwa na wabunge kwa 99.7% leo Novemba 10, 2020 jijini Dodoma.

Job Ndugai ambaye alikuwa ni mgombea pekee wa nafasi ya uspika amefanikiwa kutetea kiti chake leo na kuanza kazi rasmi kwa kuwataka wabunge kufanya kazi kwa bidii na kwa kuwasemea wananchi kero zao kwani wamechaguliwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Aidha spika Ndugai amewatoa hofu wabunge wa upinzani ambao kwa sasa ni wawili tu kwenye bunge la 12 kwa kuwahakikisha kuwa watasikilizwa na atatoa nafasi ya wao kusema.

“Kwa wabunge kutoka kambi ya upinzani najua mko wachache, tutawalinda sana na mtaishi kwa raha bila tatizo lolote na wala hamtabaguliwa” – amesema spika Ndugai.

Baada ya kuzungumza machache Mhe.Spika alishuhudia wabunge wote waliochaguliwa kwenye bunge la 12 wakila kiapo rasmi cha kuwa watumishi wa wananchi kwa miaka mitano ijayo.