Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli leo Novemba 9,2020 amemuapisha Mwanasheria mkuu wa serikali Prof.Adelardus Kilangi, Ikulu Chamwino jijini Dodoma kwenye tukio ambalo limeshuhudiwa na viongozi mbalimbali wa serikali.

Prof.Adelardus Kilangi ambaye ameteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali kwa miaka mingine mitano, anakuwa mtendaji wa kwanza wa serikali kuteuliwa na kuapishwa na Rais Magufuli kwenye muhula wa pili ya serikali ya awamu ya tano.

Prof.Adelardus amemshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini na kumpa majukumu ya kuwatumikia watanzania kwa mara nyingine kwenye nafasi hiyo huku akiomba ushirikiano kwa viongozi wote wa serikali pale itakapohitajika.

Kwa upande wa Dkt,Magufuli amemtaka Prof.Adelardus kwenda kufanya kazi kwa bidii kwenye nafasi hiyo kwa manufaa ya watanzania huku akimtaka kwenda kuisimamia vyema ofisi yake ili kesi zote zilizopo mahakamani zinazoihusu serikali ziweze kushughulikiwa haraka.

Aidha Dkt.Magufuli amesema wakuu wa Mikoa, wakuu wa Wilaya na Watendaji wengine wa serikali wasitegemee kuwa atafanya mabadiliko ya nafasi zao kwenye kipindi hiki labda zitokee changamoto kadha wa kadha hivyo amewataka kutokuwa na wasiwasi juu ya nyazfa zao.

“Pamekuwa na tabia kila serikali mpya inapoingia au awamu nyingine inapoingia watu wanakuwa na hofu hasa watendaji ndani ya serikali kwamba panatokea mabadiliko mabadiliko”

“Hakuna mabadiliko, tulianza wote tutamaliza wote mabadiliko yatakayokuwepo ni kwenye nafasi za uwaziri ambazo zenyewe tulienda kuomba upya, wapo wataokaorudi, wapo ambao hawatarudi tena”

“Inawezekana Makamu wa Rais, Spika na Naibu Spika akawa huyo huyo na Mwanasheria Mkuu amekuwa huyo huyo kwahiyo na nyinyi mtakuwa hao hao” – amesema Rais Magufuli