Shirika la hali ya hewa duniani WMO, limesema kiwango cha wastani cha hali ya joto duniani kwa mwaka huenda kikawa alau nyuzi joto moja juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya kiviwanda katika kila mojawapo ya miaka mitano ijayo.

WMO imesema kuna uwezekano wa asilimia 20 kwamba kiwango cha joto kitapindukia nyuzi 1.5 za Celsius juu ya viwango vya wastani vya mwaka 1850 hadi 1900 katika alau mwaka moja, kulingana na utabiri wake wa hali ya hewa kwa miaka mitano ijayo.

Shirika hilo la umoja wa mataifa lenye mataifa wanachama 193, limesema kipindi cha miaka mitano iliyopita kimekuwa kimevunja rekodi ya joto la miaka mitano. Limesema hali ya joto katika miaka mitano kuanzia 2020 hadi 2024 inaweza kuwa kati ya nyuzi 0.91 hadi 1.59 juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda.